Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 11,2025 jijini Dodoma kuhusu kuanza mchakato wa kujaza nafasi za upungufu wa watumishi katika taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi wa umma nchini.
…..
SERIKALI imeelekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuanza mara moja mchakato wa kujaza nafasi za upungufu wa watumishi katika taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi wa umma nchini.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 11,2025 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa serikali imekamilisha mchakato wa ajira zote za mwaka 2024/25 kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa huduma hauathiriki kutokana na uhaba wa rasilimali watu.
“Katika mwaka wa fedha 2025/26, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliidhinisha nafasi 41,500 za ajira mpya kwa taasisi mbalimbali, zikiwemo nafasi 12,176 za walimu na nafasi 10,280 za kada za afya, ambapo utekelezaji wake unaanza mara moja,” amesema Mkomi.
Aidha ameeleza kuwa ili kupunguza gharama kwa waombaji wa ajira, kuongeza uwazi wa mchakato, na kuharakisha upatikanaji wa watumishi wenye sifa, waajiri wametakiwa kutoa ushirikiano na kuruhusu waombaji kufanya usaili katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
“Ili kuhakikisha Sekretarieti ya Ajira inatekeleza jukumu hili ipasavyo, waajiri wote wanaelekezwa kutoa ushirikiano. Pia wale waliokasimiwa madaraka ya kuendesha mchakato wa ajira kwa baadhi ya kada wanapaswa kufanya usaili mara moja ili kujaza nafasi walizoidhinishiwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma,” alisisitiza.
Aidha, Mkomi amesema kwa lengo la kupunguza gharama na kurahisisha mchakato, zoezi la usaili litafanyika katika kila mkoa Tanzania Bara, na vituo maalum vitaandaliwa upande wa Zanzibar ili kutoa fursa kwa waombaji kutoka maeneo husika kushiriki kwa urahisi.
“Waombaji watakaofaulu usaili lakini hawatapangiwa kazi mara moja, watahifadhiwa kwenye Kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira na watapangiwa kazi kwa kadri nafasi mpya zitakavyopatikana, katika taasisi mbalimbali nchini,” amesema Mkomi.
Hata hivyo, ameiongeza kuwa barua za kupangiwa vituo vya kazi kwa waombaji watakaofaulu usaili zitapatikana kupitia Mfumo wa Ajira Portal kwa akaunti binafsi za wahusika, ili kuondoa changamoto ya ucheleweshaji na upatikanaji wa taarifa.