VIJANA wa taasisi ya ‘Nguvu kazi Kizimkazi’ na wenzao kutoka mikoa 10 wakiwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro Uhuru mara baada ya kupandisha bendera ya mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, kumuunga mkono katika mbio zake za kuwania nafasi hiyo hivi karibuni. (NA MPIGA PICHA MAALUM).
NA MWANDISHI WETU
KATIBU MTENDAJI wa Taasisi ya ‘Vijana Nguvu Kazi Kizimkazi Zanzibar, Abusufiani Yakuti Juma, amesema mafanikio ya kupandisha Bendera Maalum ya Dk. Samia Suluhu Hassan juu ya Kilele cha Mlima Kilimanjaro ni alama ya umoja, uzalendo na kuunga mkono juhudi viongozi hao wawili wanaosimamia maendeleo ya taifa.
Abusufiani aliyeongoza msafara wa vijana hao na kufanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru Oktoba 7, mwaka huu, alieleza kuwa hatiua hiyo ni ishara ya uzalendo na kuunga mkono juhudi za Dk. Samia katika kuleta maendeleo na kuimarisha umoja wa kitaifa kupitia sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Alifafanua kuwa hatua hiyo pia ni sehemu ya kampeni ya vijana wa Tanzania kushirikiana katika matendo yanayoinua heshima ya taifa, kuwaenzi viongozi kwa vitendo lakini pia kutoa wito kwa vijana nchini kuendeleza umoja, amani na mshikamano kama sehemu ya kuenzi azi kubwa inayofanywa na serikali katika uongozi wa Dk. Samia.
“Kupandisha bendera maalum ya Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro ni alama ya umoja, uzalendo na kuunga mkono viongozi hao wawili wanaosimamia maendeleo ya taifa”, alisema Abusufiani.
Aliongeza kuwa hatua hiyo limeandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na vijana wengine kutoka mikoa 10 tofauti ya nchi, likiwa na kaulimbiu ya ‘Dk. Samia na Dk. Mwinyi wanatosha — Kura yangu na kura yako kwa maendeleo yetu, Oktoba tunatiki’.
Abusufiani alitaja mikoa iliyotoa vijana walioshiriki kupandisha bendera hiyo kuwa ni Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Kilimanjaro, Manyara na Kigoma na kuwapongeza wadau wote waliofanikisha zoezi hilo.
“Tumeweka historia hii si kwa kushindana, bali kwa kuonesha mshikamano na imani kwa viongozi wanaoleta mageuzi makubwa ya maendeleo nchini hivyo vijana tunapaswa kutimiza wajibu wetu kwa nchi na viongozi wetu”, alisema Abusufiani.
Aliongeza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kujenga taifa, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani, kuhamasisha umoja na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.