Featured Kitaifa

REA YATOA RAI KWA WANANCHI KUWATUMIA MAFUNDI WENYE LESENI ILI KUJIUNGANISHA NA HUDUMA YA UMEME

Written by Alex Sonna


Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wenzao wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wameendelea na zoezi la uhamishaji Wananchi wa wilaya ya Meatu, Itilima na Busega mkoani Simiyu kujiunganisha na huduma ya umeme (Wiring) lakini wawatumie, Mafundi wenye leseni na sifa ya kufanya kazi hiyo.

Wito huo, umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka REA, Bi. Jaina Msuya kwa nyakati tofauti katika vitongoji vya Mwamango; Ushashi na Ibelambasa wilayani Itilima, kitongoji cha Maduakni, wilayani Meatu na kitongoji cha Maguye na Mwabasabi wilayani Busega baada ya uwepo wa viashiria vya mafundi wasio na sifa (Vishoka).

Bi. Jaina amesema kufanya ‘wiring’ na kujiunga na huduma ya umeme ni suala binafsi na ni maelewano kati ya mteja na fundi lakini; Wananchi wanatakiwa kuwapa kazi mafundi mwenye sifa (Fundi mwenye leseni).

“Fundi ambaye hana leseni (Kishoka); hawezi kukufanyia kazi ya ‘wiring’ pamoja na kukamilisha ombi lako la kujiunga na huduma ya umeme ila fundi mwenye leseni atakufanyia wiring na kuomba kujiunga na huduma ya umeme TANESCO kupItia simu yako na kwa bei ya Serikali (Shilingi 27,000)” amesema Bi. Jaina.

Bi. Jaina ameongeza kuwa ni jukumu la Mwenyekiti wa Kitongoji kumuomba mkandarasi ili awape mafundi wenye sifa baada ya kukamilika kwa Miradi kwenye vitongoji vyao kwa kufanya mkutano wa pamoja kati ya Wananchi na mafundi wa mkandarasi.

Naye Mhandisi, Deusdedit Mzanze, Meneja wa Miradi ya REA mkoa wa Simiyu amesema wapo Watu ambao siyo waaminifu ambao wamekuwa wakipita kwa Wananchi na kuwatapeli fedha kwa kuwaambia kuwa watafanya ‘wiring’ pamoja na kuwaunganisha na huduma ya umeme kutoka TANESCO.

“Atakayekuja na kukwambia nipe fedha zako (Shilingi 27,000) ili nikakuunganishe na huduma ya umeme, huyo ni tapeli, usikubali, maombi yanapaswa kuombwa, kupitia simu yako na TANESCO watakutumia namba ya malipo (Control Number)” amesisitiza, Mhandisi Msanze.





About the author

Alex Sonna