Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025, likiahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa ubunifu, kasi na ufanisi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania na wateja wake wa kimataifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa wiki hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kujitathmini na kuimarisha uhusiano kati ya shirika hilo na wateja wake.
“Wiki hii inatukumbusha wajibu wetu wa msingi wa kumweka mteja mbele kama kiini cha mafanikio ya TTCL. Tunajitathmini, tunasikiliza, na tunajifunza kutoka kwa wateja wetu,” amesema Bi. Moshi.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja hufanyika duniani kote kila mwaka wiki ya kwanza ya Oktoba. Kwa mwaka huu, TTCL inasherehekea kuanzia Oktoba 6 hadi 10, 2025 chini ya kaulimbiu isemayo “Mission: Possible.”
Bi. Moshi amesema kaulimbiu hiyo imechaguliwa kuonyesha dhamira ya TTCL ya kuona kila changamoto kama fursa ya kuboresha huduma na kutafuta suluhisho la kudumu kwa manufaa ya wateja.
“Tutakuwa wabunifu, wenye bidii na maono. Kila mmoja wetu atakuwa sehemu ya suluhisho, na kwa pamoja tutahakikisha kila mteja anathaminiwa na kuhudumiwa kwa ubora wa hali ya juu,” amesisitiza.
Amesema TTCL imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini, ikiwa ni pamoja na kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi kufikia wilaya zote za Tanzania, pamoja na ujenzi wa minara 1,400 vijijini ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano bila vikwazo.
Aidha, amesema kupitia huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako”, TTCL inaendelea kuwapatia Watanzania huduma ya intaneti ya kasi na uhakika inayokidhi viwango vya kimataifa.
Bi. Moshi ameongeza kuwa TTCL itaendelea kuwekeza katika teknolojia bunifu, kuboresha mifumo ya huduma kwa wateja na kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora popote walipo.
Amewahimiza wateja waendelee kutumia Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachofanya kazi saa 24, pamoja na mitandao ya kijamii na maduka ya TTCL nchini kote, kupata ushauri na taarifa muhimu.
“Tutaendelea kuwa karibu na wateja wetu, kuwaheshimu, na kuhakikisha wanapata huduma bora zenye ufanisi na thamani,” amesema.
Bi. Moshi amewashukuru wateja wote walioliweka TTCL kama chaguo lao la mawasiliano kwa miaka mingi na kuwataka waendelee kushirikiana na shirika hilo katika safari ya maendeleo ya kidijitali.
“Wateja wetu ndiyo msingi wa mafanikio yetu. Tutaendelea kuwa bega kwa bega nao kufanikisha azma yetu ya pamoja — Mission: Possible,” alisisitiza kabla ya kutangaza rasmi uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ya TTCL kwa mwaka 2025.