Featured Kitaifa

MAFUNZO YA MADAKTARI BINGWA YASAIDIA KUOKOA MAISHA MKOANI DODOMA

Written by Alex Sonna

 

Na, WAF-Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema kambi ya madaktari bingwa kupitia mafunzo kwa wataalam imewezesha kuokoa maisha ya wengi kutokana na uwezo waliojengewa wa kushughulikia wagonjwa wa dharura na majeruhi wa ajali kwa haraka na kwa ufanisi.

Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Oktoba 06, 2025 wakati akiwapokea wataalam wa afya wabobezi 42 wakiwepo Madaktari Bingwa na Wauguzi Bobezi ambao watafanya kazi ya kutoa huduma kwenye halmashauri za wilaya saba (7) za mkoa wa Dodoma.

“Ubunifu huu uliofanywa na Serikali wakuwajengea uwezo wataalam wetu ngazi ya msingi, lakini pia kuanzishwa kwa majengo ya dharura sisi tumeona matunda yake, kwani hivi karibuni tulipata ajali katika wilaya yetu ya Chemba kutokana na utaalam ambao mliwawezesha watu wetu, kuwahudumia majeruhi wote na kuwafikisha ngazi ya RRH wakiwa salama,” amesema Mhe. Senyamule.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Afya Bi. Subira Said, amesema shabaha ya zoezi hilo ni kusogeza huduma karibu na jamii, kuwajengea uwezo wataalam ngazi ya msingi na kuwatambua wagonjwa ambao matatizo yao yanahitaji rufaa kwenda mkoa, kanda au hata taifa.

“Zoezi hili limeleta tija kwani kati ya Mei 2024 hadi Juni 2025, jumla ya wagonjwa 230,524 walipata huduma ambapo kati ya hao 16,570 walipatiwa huduma za upasuaji huku watoa huduma 15,019 walipatiwa mafunzo elekezi kazini,” ameanisha Bi. Subira.

Awali akitoa taarifa ya mkoa, Mganga Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt. Thomas Rutachunzigwa amesema katika awamu zilizopita mkoa wa Dodoma uliwafikia wanamchi 7,200, huku akisema kuwa katika awamu hii wanatazamia kuwafikia wananchi zaidi ya 8000 kutokana na zoezi hilo kulitangaza vya kutosha.

Mkoa wa Dodoma umepokea Watalam Bingwa na Bobezi wapatao 42 ambao ni wa kada za upasuaji, magonjwa ya watoto na watoto wachanga, wanawake na uzazi, Usingizi na ganzi salama, magonjwa ya ndani, kinywa na meno pamoja na wauguzi wabobezi.

About the author

Alex Sonna