Featured Kitaifa

DOLA MILIONI 6 ZAKAMILISHA UJENZI WA VIHENGE VYA KISASA SUMBAWANGA

Written by mzalendoeditor

Vihenge vya kisasa nane vilivyokamilika kujengwa na Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga katika eneo la Kanondo Manispaa ya Sumbawanga vyenye uwezo wa kubeba tani 20,000 za mazao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (katikati) akiongea na Meneja wa NFRA Sumbawanga Marwa Range (wa pili toka kushoto) juzi wakati alipokagua mradi wa ujenzi wa vihenge na ghala la kisasa vilivyokamilika katika eneo la Kanondo Manispaa ya Sumbawanga.

Meneja wa NFRA Kanda ya Sumbawanga Marwa Range (katikati) akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (wa pili toka kulia) juzi wakati wa 
ziara ya  kagua ghala jipya lenye uwezo wa kubeba tani 5,000 za mazao. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (wa kwanza kushoto) akisikiliza maelezo ya fundi wakati alipokagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Matanga Manispaa ya Sumbawanga kinachojengwa kutokana na fedha za tozo ya miamala ya mawasiliano.  Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa)

……………………………………………..

Na. OMM Rukwa

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Sumbawanga imefanikisha ujenzi wa vihenge nane na ghala moja la kisasa vitakavyoongeza uwezo wa kuhifadhi mazao tani 25,000 kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 6.019.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliyetembelea mradi huo uliopo eneo la Kanondo katika Manispaa ya Sumbawanga alisema kukamilika kwake ni mafanikio kwa wakulima wa Rukwa na Taifa kuwa na uwezo wa kuhifadhi nafaka kisasa.

“Mradi huu utakuwa mkombozi kwa Taifa kuhifadhi akiba yake ya chakula kwa njia ya kisasa ambapo wananchi wa Rukwa ndio wanufaika wakubwa kutokana na vihenge hivi kuwa hapa Sumbawanga” alisema Mkirikiti.

Akitoa taarifa ya mradi huo , Mhandisi Mkazi toka kampuni ya M/s Unia Araj  ya Poland Mhandisi Haruna Kalunga alisema mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 2020 umehusisha ujenzi wa vihenge nane, majengo 6,ghala moja, mzani mmoja na uzio  kuzunguka eneo hilo.

Mhandisi Kalunga aliongeza kusema vihenge hivyo vya kisasa vikubwa vipo sita na vidogo viwili pamoja na miundombinu yake vina uwezo wa kubeba tani 20,000 ambapo ghala la kuhifadhia mazao limekamika pia likiwa na uwezo wa kubeba tani 5,000  na kuwa mradi huo umekamilika mwezi Machi mwaka huu na majaribio tayari yamefanyika mwezi Aprili mwaka huu.

“Mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa Dola za Kimarekani 5,417,459 sawa na asilimia 90 ya fedha zote za mkataba ambazo ni Dola za Kimarekani 6,019,399” alieleza Mhandisi Kalunga.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kalunga alitoa ombi kwa serikali kupitia VETA kuwarasimisha vijana wa kitanzania wapatao 60 ambao walioshiriki kazi za ujenzi wa vihenge vyote na miundombinu yake kutokana na uwezo na uzoefu wao.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunaomba vijana wazalendo walioshiriki ujenzi wa mradi huu warasimishwe na VETA kupitia mpango wa urasimishaji ujuzi nje ya mfumo rasmi” alihitimisha taarifa yake Mhandisi Kalunga.

Naye Meneja wa NFRA Kanda ya Sumbawanga Marwa Range alisema kufuatia kukamilika kwa mradi huo Wakala tayari umeanza kutumia miundombinu hiyo kuhifadhi mazao na kuwa utasaidia kuboresha hali ya uhifadhi nafaka kwa matumizi ya Taifa.

Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kupitia mpango wa Storage Capacity Expansion Project (SCEP) ilipokea mkopo wa fedha wenye masharti mepesi toka serikali ya Poland kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia mazao na miundombinu yake kwenye mkoa wa Rukwa.

About the author

mzalendoeditor