Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI NDEJEMBI ATAKA UWAJIBIKAJI KWA WAKAGUZI WA NDANI NCHINI

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka Wakaguzi wa Ndani kusimamia kwa weledi ukaguzi wanaoufanya ili kuweza kuisaidia Serikali kuepukana na hasara ambazo imekua inapata au kusubiri kuvumbuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ndejembi ameyasema hayo alipokua akizungumza na Wakaguzi wa Ndani wakati akifungua mkutano wao jijini Tanga ambapo amewaahidi kuwa Serikali itahakikisha inafanyia kazi maboresho waliyoomba wapatiwe ili kuwafanya kuwa miongoni mwa idara rasmi za Serikali.

“Wakati tunapohitaji kutambulika rasmi kama Idara yenye nguvu kwenye Taasisi za Umma basi tusisahau wajibu wetu kama wakaguzi wa ndani, mna wajibu mkubwa sana wa kuisaidia Serikali. Haya yote mnayoyaona kwenye ripoti za CAG ni kufeli kwa kitengo cha wakaguzi wa ndani kuyaona hayo, hivyo niwaombe muisaidie Nchi yenu.

Lakini nyie wakaguzi wa ndani ndio mnaosaidia uwajibikaji na utawala bora kwa watumishi wa umma, Sasa Wakati sisi tunaenda kufanya maboresho ya Taasisi yenu hebu na nyie kahakikishe uwajibikaji unakuwepo kwenye ofisi za umma,” Amesema Ndejembi.

Amesema Serikali itaendelea kuheshimu na kutoa ushirikiano kwa wakaguzi wa ndani nchini na kwamba kufikia mwaka 2023 kero na changamoto ambazo zinawakabili wakaguzi wa ndani zitakua zimefanyiwa kazi na kuifanya Idara hiyo kuwa yenye nguvu katika taasisi za umma.

About the author

mzalendoeditor