TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewateua Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi, kugombea nafasi ya urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza leo Agosti 27, 2025 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, amesema wagombea waliopendekezwa na CCM wametimiza masharti yote ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuthibitishwa rasmi kuwania nafasi hizo.
“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inawateua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji mstaafu Mwambegele.
Uteuzi huo unawafanya Samia na Nchimbi kuingia rasmi katika kinyang’anyiro cha urais kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambao kampeni zake zinatarajiwa kuanza kesho Agosti 28, 2025.