Featured Kitaifa

SAU KUTOA AJIRA MILIONI 10 NDANI YA MIAKA MITANO

Written by mzalendo
Mgombea wa Urais kupitia tiketi ya  Chama cha Sauti ya Umma (SAU),Majalio Kyara amesema endapo atapewa ridhaa ya kuchaguliwa kugombea kiti hicho,serikali ya chama hiko imepanga kutoa ajira milioni 10 ndani ya miaka mitano.
Kyara ambaye ameongozana na mgombea Mwenza Satia Mussa Bebwa,amesema atazitoa ajira hizo ndani ya kipindi ambacho watakuwa madarakani na kuondoa kabisa changamoto hiyo.
Amefafanua zaidi ya kuwa kwenye hilo pia  anakwenda kurudisha heshma ya walimu kwa kuwapa mazingira wezeshi ambayo yatamuwezesha mwalimu kufundisha vizuri wanafunzi katika shule mbalimbali hapa nchini.
“Sau inakwenda kuondoa unyonge kwa wananchi hivyo tunakwenda kutekeleza vipaumbele vyetu kwa ufasaha ambavyo ni Kilimo,Afya na Ajira,”amesema Kyara.
Mbali na hilo wanakwenda kuondoa gharama za umeme ili kuwafanya wananchi watumie Nishati safi ya kupikia ili waweze kutunza mazingira katika maeneo mbalimbali na kuongeza wataleta kampuni ambayo itakuwa inatengeneza majiko ya kutumia teknolojia ya kisasa.
“Tutaliangalia sana suala la vijana wa kiume kwa sababu ili waweze kupata kazi za kufanya ili waweze kujikwamua kiuchumi,”amesema Kyara.
Amesema wamepanga kuzindua Ilani yao wiki ijayo na kuongeza kuwa wamejipanga pia kurudisha mchakato wa katiba mpya ambayo itakubalika na wananchi.

About the author

mzalendo