Featured Kitaifa

MGOMBEA URAIS DP ACHUKUA FOMU YA URAIS INEC

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma

Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Siasa cha Democratic Party (DP),Abdul Mluya, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi moja kati ya vipaumbele vyao ni suala la Afya, ambapo kinamama watajifungua bure na mtoto atapewa lishe kwa miezi mitatu.

Mluya ambaye amembatana na mgombea mwenza Saodun Abraham Khatibu amesema hayo leo Agosti 13,2025 mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi zilizopo Njedengwa Jijini. Dodoma.

Aidha ameongeza kuwa kupitia kipaumbele hicho cha afya marehemu hatodaiwa hela ya matibabu, ndugu watapewa mwili ili wakazike na kwenye kilimo watahimiza kilimo cha umwagiliaji.

Amesmea kipaumbele chao kingine ni kwenda kusimamia suala la Kikokotoo.

“Suala la Kikokotoo kwa watumishi imekuwa changamoto kubwa sana kwa watumishi hivyo DP inakwenda kulifanyia kazi suala hilo ili watumishi waweze kupata mafao yao bila changamoto yeyote.
Tunakwenda kufuta kilio cha Kikokotoo kwa watumishi,haiwezekani mtu afanye kazi ndani ya miaka 33 halafu alipwe mafao sh milioni 13 hadi 14 hilo tunakwenda kuliondoa,”amesema Mluya.

Amesema serikali ya DP itakwenda kuwajengea nyumba watumishi ambao wamekaa ofisini zaidi ya mwaka bila kashfa ya kosa lolote lile ili kusaidia kuondoa rushwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mbali na hayo pia amesema DP itashughulikia na kuboresha maslahi ya Jeshi la Magereza pamoja na majeshi mengine ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora na kuongeza kuwa wataboresha pia suala zima la Magereza ya wafungwa hapa nchini.

About the author

mzalendo