Featured Kitaifa

WAZIRI BASHUNGWA AIBUA ‘MADUDU’ WILAYANI BUNDA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Mhe. Innocent Bashungwa akiongea na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda katika ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Halmashauri hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Innocent Bashungwa akitoa maagizo kwenye kikao na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mkoani Mara.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi,akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Innocent Bashungwa  na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mkoani Mara.

Baadhi ya Viongozi walishiriki kikao ha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakisikiliza maagizo kwenye kikao na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mkoani Mara

………………………………..

Na Angela Msimbira, OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema kumekuwa na mdororo mkubwa wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara hali inayopelekea kucheleweshwa kwa maendeleo katika halmashauri hiyo.

Akizungumza kwenye kikao na menejimenti pamoja madiwani walipotembelea halmashauri kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa, Waziri Bashungwa amesema kwenye suala la ubovu wa miradi imeonekana kwenye ujenzi wa jengo la utawala vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 283. 83 vimelipiwa, lakini havijapokelewa na halmashauri na havijulikani vilipo.

Ameendelea kufafanua kuwa, kwa upande wa Mhandisi wa Mradi SUMA JKT kutokuwepo kwenye eneo la mradi huo kwa muda mrefu hali inayopelekea jengo hilo kutokamilika kwa wakati na si jambo jema.

Bashungwa amefafanua kuwa,pia kumekuwa na ucheleweshaji na usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Waziri Bashungwa amesema, inashangaza kwenye upande wa kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,halmashauri kufanya maamuzi bila idhini ya bodi ya wazabuni zaidi ya shilingi milioni 108. 5 na kushindwa kuchukua hatua kwa mapato ambayo hayakuwasishwa benki zaidi ya shilingi milioni 144. 1.

Sambamba na kushindwa kukusanya mapato yenye thamani ya shilingi milioni 154. 6 sawa na asilimia 11 ya lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1. 4.

Waziri Bashungwa amesema, hoja nyingine kubwa ni halmashauri kushindwa kupeleka fedha za mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo ya shilingi milioni 260. 7 hivyo ameitaka kuhakikisha inapeleka fedha kulingana na bajeti iliyopangwa.

Amesema kuwa, pia halmashauri ilifanya malipo bila kudai risiti za kielektroniki zaidi ya shilingi milioni 782.

About the author

mzalendoeditor