
Na Gideon Gregory, Dodoma
Mgombea Urais kupitia Chama cha Makini Coaster Jimmy Kibonde leo Agosti 10,2025 amefika katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo Njedengwa Jijini Dodoma akiwa na mgombea mwenza Azza Haji Suleiman.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za tume hiyo mara baada ya kuchukua fomu aliyokabidgiwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, Kibonde ametaja vipaumbele vitatu endapo atashinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29,2025.
Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na Elimu, Kilimo na Afya ambavyo vyote hivyo watavitekeleza kwa wananchi ili kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake.

“Kwenye elimu kila mtanzania lazima asome kwa sababu ukiinyima jamii elimu utasababisha washindwe kupiga hatua kwenye maendeleo ya kiuchumi,”amesema.
Kuhusu suala la Afya amesema wataanzisha bima ya afya itakayoitwa Bima Makini ambayo kila mmoja atapaswa kuwa nayo ili aweze kupata matibabu pale wanapopata changanoti za kiafya.
Mbali na hilo amesema kwenye suala la kilimo kila mtanzania atapariwa hekari tano pamoja na Trekta kwa ajili ya kuendeleza kilimo ili waweze kujiinua kiuchumi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Leo vyama vitatu vya siasa wagombea vinatarajia kuchukua fomu za kugombea nafasi ya kiti cha Urais katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) zilizopo Njedengwa jijini hapa ambavyo ni CHAMA cha MAKINI, NLD na UPDP