Featured Kitaifa

VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA NA WAFUASI WAO WAASWA KUFANYA KAMPENI ZA KISTAARABU

Written by mzalendo

Mwenyekiti wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akifungua mkutano wa kitaifa wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi na vyama vya siasa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 Leo Julai 27,2025 Jijini Dodoma.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa kwenye mkutano wa kitaifa wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi na vyama vya siasa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Na Gideon Gregory, Dodoma

Mwenyekiti wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao kufanya kampeni za kistarabu na kuepuka vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi.

Jaji Mwambegele ametoa rai hiyo leo Julai 27,2025 Jijini Dodoma, wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi na vyama vya siasa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 uliokwenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Kura yako haki yako jitokeze kupiga kura”.

“Kipindi cha kampeni kunakuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi,”amesema.

Aidha, amewasihi kusoma sheria, kanuni na maelekezo kuhusu uchaguzi mkuu ili ushiriki wao katika mchakato huo uweze kufanyika kwa kuzingatia masharti na matakwa husika.Β 

Sambamba na hayo amesema kuwaΒ Tume inawahakikishia kuwepo kwa uwanja sawa kwa vyama vyote wakati wa kampeni kwa kuhakikisha kila chama kitafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba itakayokuwa imepitishwa na kamati ya ratiba ngazi ya Taifa inayoratibu ratiba ya kampeni ya wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, kamati ya jimbo inayoratibu ratiba ya wagombea wa ubunge na kamati ya kata inayoratibu ratiba ya wagombe wa udiwani.

Pia ameongeza kuwa ili kuwa na uwazi katika zoezi la Uchaguzi Mkuu, Tume imekuwa ikiwashirikisha wadau wa uchaguzi, mkiwemo ninyi, katika hatua mbalimbali za mchakato wa Uchaguzi. Mathalani, leo tunakutana nanyi Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na kuanzia tarehe 30 Julai, 2025 hadi tarehe 03 Agosti, 2024 tutakuwa na vikao na wadau mbalimbali.

“Aidha, kikao hiki siyo kwamba ndiyo mwisho wa kukutana nanyi, tutakuwa tunafanya vikao vya aina hii au vya aina nyingine katika kipindi hiki cha uchaguzi,”amesema.Β 

Akiwasilisha mada kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mkurugenzi wa uchaguzi wa INEC Ramadhan Kailima amesema kuwa tume imeweka utaratibu wa namna ya wafungwa kwa Tanzania Bara na wanafunzi kwa upande wa Zanzibar pamoja na mahabusu watakavyoruhusiwa kupiga kura siku ya uchaguzi.

Ameongeza kuwa Tume imeweka utaratibu wa kushirikisha vyama vya siasa katika mchakato mzima ili kuweka uwazi, hivyo wanatarajia kupata ushirikiano kutoka kwao na kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa wa amani.

About the author

mzalendo