Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeweka wazi ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, utakaohusisha uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge, pamoja na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara.
Ratiba hiyo imetangazwa leo Julai 26,2025 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele ambapo hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mapema ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia kama ilivyoainishwa kwenye Katiba na sheria za nchi.
“Ratiba Muhimu ya Uchaguzi: Utoaji wa Fomu za Uteuzi kwa Wagombea wa Urais na Makamu wa Rais:Agosti 9 hadi Agosti 27, 2025, Siku ya Uteuzi wa Wagombea (Rais, Makamu wa Rais, Ubunge na Udiwani):Agosti 27, 2025, Kipindi cha Kampeni Tanzania Bara:Agosti 28 – Oktoba 28, 2025, Kipindi cha Kampeni Zanzibar:
Agosti 28 – Oktoba 27, 2025
(Kupisha upigaji kura wa mapema), Siku ya Kupiga Kura Kitaifa:
Jumatano, Oktoba 29, 2025″, amesema Jaji Mstaafu Mwambegele.
Aidha, Jaji Mstaafu Mwambegele ameeleza kuwa kutakuwa na vituo vya kupigia kura 99,911 nchini kote, kati ya hivyo vituo 97,349 vitakuwa Tanzania Bara na 2,562 visiwani Zanzibar, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.49 kutoka vituo 81,467 vilivyotumika mwaka 2020.
Katika hatua nyingine ya kuhakikisha uadilifu wa uchaguzi, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) , Ramadhani Kailima, amekabidhi orodha ya watu 8,703 waliojiandikisha zaidi ya mara moja katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Jeshi la Polisi, kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wawakilishi kutoka vyama kumi na nane walihudhuria hafla hiyo na kueleza utayari wao kushiriki uchaguzi kwa amani na kwa mujibu wa sheria. Wamepongeza hatua ya INEC kuweka wazi kalenda ya uchaguzi mapema, wakisisitiza umuhimu wa elimu ya mpiga kura kuendelea kutolewa.