Featured Kitaifa

RC RUKWA: HATUTAKI VYAMA VYA USHIRIKA OMBAOMBA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (pichani) amevitaka vyama vya ushirika mkoani humo kujiimarisha kiuchumi ili viachane na mikopo isiyo na tija hatua inayowafanya washindwe kuhudumia wakulima. Ametoa kauli hiyo leo mjini alipofungua mkutano maalum wa vyama vya ushirika Rukwa

Sehemu ya wanachama wa vyama vya ushirika kutoka wilaya zote za mkoa wa Rukwa wakiwa kwenye mkutano maalum Chama Kikuu cha Ushirika cha Ufipa kilichofanyika mjini Sumbawanga.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ufipa Mkoa wa Rukwa Bw. Adabeth Mbuyani akizungumza kwenye mkutano mkuu maalum wa vyama vya ushirika leo mjini Sumbawanga leo.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa).

……………………………………………….

Na. OMM Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amewashauri viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Ufipa kujiimarisha kiuchumi ili kuachana na mtindo wa kutegemea wahisani kwa mikopo yenye riba kubwa hatua inayofifisha uwezo wa kuhudumia wakulima.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa rai hiyo leo (05 Mei, 2022) wakati akifungua mkutano maalum wa vyama vya ushirika mkoa huo mjini Sumbawanga na kusisitiza kuwa uimara wa chama kikuu kuwa na mtaji wake ndio nguzo ya kuhudumia wakulima.

“Ili mfaidi matunda ya ushirika lazima mtumie uwepo wa chama kikuu cha ushirika cha Ufipa kupata nguvu za kiuchumi kuwezesha wana ushirika kupata suluhisho la kero za wakulima” alisisitiza Mkirikiti.

Mkirikiti aliongeza kusema ni wakati muafaka kwa wanaushirika kuelimishwa umuhimu wa mfumo wa stakabadhi za ghala kwa mazao ya ufuta na soya ili wakulima wa Rukwa wawe na uhakika wa bei nzuri itakayowapa kipato cha uhakika na kuondokana na utegemezi wa zao la mahindi pekee kama zao la biashara.

Amepongeza mikakati wa Chama Kikuu cha Ushirika Ufipa wa kuanza kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa zao la soya msimu huu na kwamba wahakikishe Maafisa ushirika wanatoa elimu kwa wakulima.

Kuhusu mfumo wa stakabadhi za ghala, Mkirikiti amewataka Maafisa Ushirika wa Halmashauri kutoa elimu ili wakulima wengi waulewe na kuepuka vishawishi vya wasioutakia mema mfumo huo .

“Vita ya kupanga mfumo wa stakabadhi za ghala siyo ndogo, lazima mjipange kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo kuwatumia watu wenye uzoefu” alisema Mkirikiti.

Katika hatua nyingine Mkirikiti amevitaka vyama vya msingi vya ushirika kuona fursa ya zao la ngano, alizeti na ufuta kwa kuhamasisha wakulima ili wawe na mazao mbadala yatakayoongeza kipato chao ikiwemo kuanzisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Mkirikiti amevitaka vyama vya ushirika mkoani Rukwa kutambua mahitaji ya wakulima kwa sasa kuwa ni moja upatikanaji wa mbolea kwa wakati, mbili soko la mazao la uhakika, tatu elimu ya kilimo chenye tija , nne umuhimu wa bima ya mazao na tano kilimo endelevu cha umwagiliaji .

Akizungumza kwa niaba ya wanaushirika Mzee Zeno Nkoswe alishukuru uwepo wa bodi mpya ya Chama Kikuu cha Ushirika Ufipa na kuwa imeanza kuonesha mwanga wa kuwezesha wakulima kuwa na uhakika na kilimo chao kwa kutafuta pembejeo na masoko.

Naye Mkuu wa Mkoa Mstaafu Ludovick Mwananzila alisema alishiriki miaka mitatu iliyopita katika ufufuaji wa Chama Kikuu hicho cha Ufipa na kuwa sasa kimelenga kuwahudumia wakulima kujikomboa kiuchumi.

Mwananzila aliongeza kusema jukumu la ushirika wa kisasa ni kuleimisha wakulima watambue haki na ushiriki wao katika ushirika ikiwemo kupata manufaa ya kiuchumi.

Akitoa taarifa ya Chama Kikuu cha Ushirika Ufipa Mwenyekiti wake Adabeth Mbuyani alieleza kuwa wamefanikiwa kupata mkopo wa pembejeo za kilimo wenye thamni ya shilingi Bilioni 1.7 kwa vyama vya ushirika vya msingi 40 kati ya 54 ambao umesaidia wakulima.

Mbuyani aliongeza kuwa katika msimu wa 2021/22 chama kikuu hicho kimelenga kuingiza mazao ya wakulima kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala kutokana na mwongozo wa Wizara ya Kilimo na zao la soya litaanza msimu huu.

Aidha, Mbuyani alitoa ombi kwa serikali kurejesha kwa maghala yaliyokuwa yakitumika na ushirika ili yasaidie wakulima wa mkoa wa Rukwa.

About the author

mzalendoeditor