Kitaifa

BABA MZAZI WA MBWANA SAMATTA AFARIKI DUNIA

Written by mzalendoeditor

NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefiwa na baba yake mzazi, Ally Samatta Pazi (82) aliyefariki dunia mapema leo asubuhi nyumbani kwake, Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Mohamed Samatta – baba yake amefariki baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu na taratibu za mazishi zinasubiri mtoto mwingine wa marehemu, Mbwana Samatta anayeishi Ugiriki kuwasili.
Samatta ambaye ni Kamishna Msaidizi Mstaafu wa Jeshi la Polisi Tanzania, enzi zake alikuwa mchezaji mzuri wa nafasi ya ushambuliaji ambaye alichezea hadi timu ya taifa ya Tanzania, Taia Sars kuanzia mwaka 1964 hadi 1965.

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amefiwa na baba yake mzazi leo Mbagala Kuu, Dar es Salaam.

Alizaliwa Oktoba 28 mwaka 1943 na umaarufu wake katika soka ulianza alipokuwa anasoma sekondari ya Mzumbe mkoani Morogoro kwenye michezo ya Shule kati ya mwaka 1961 na 1962 na mwaka 1963 akaajiriwa Jeshi la Polisi Tanzania na kuanza kuchezea timu ya jeshi hilo Jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1965 alisajiliwa na Cosmopolitan ya Dar es Salaam aliyoichezea hadi mwaka 1966 akarejea Polisi na mwaka 1968 akasajiliwa na Sunderland, sasa Simba SC ambako alicheza kwa miezi kadhaa kabla ya kurejea Polisi kufuatia kuhamishiwa kikazi mkoani Mara.
Alicheza Polisi Mara kwa mwaka mmoja hadi 1969 alipohamia kikazi Bukoba na kiuchezea Polisi Kagera hadi mwaka 1973 alipohamia Polisi Morogoro, hadi 1975 akarejea Polisi Mara hadi 1980 akahamia Polisi Shinyanga hadi alikodumu kwa miezi michache akahamishiwa Polisi Tanga ambako alistaafia mwaka 1992.
Mungu ampumzishe kwa Amani marehemu Ally Samatta Pazi. Amin.

About the author

mzalendoeditor