Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi James Jumbe Wiswa leo Julai 2, 2025 amerejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu katika ofisi za CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi Wiswa amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu limeenda vizuri na kwa utulivu mkubwa bila changamoto yoyote.
“Leo nimekuja kwa mara ya pili, hatua ya kwanza ilikuwa ni uchukuaji wa fomu, nimejaza fomu, na leo ni siku ya urejeshaji. Tumekamilisha hatua ya awali ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu. Zoezi limeenda vizuri. Kimsingi, mimi binafsi nimeona zoezi limeenda vizuri na wala sijasikia kwa mtia nia ya ubunge mwingine kama kulikuwa na changamoto yoyote katika hatua hii,” amesema Mhandisi Jumbe.
Mhandisi Jumbe amepongeza uongozi wa CCM Wilaya kwa kuweka mazingira rafiki kwa watia nia na wagombea, akieleza kuwa taratibu zimekuwa rahisi na hazichukui muda mrefu.
“Unapofika kuchukua fomu unapewa control number, unalipia, unakabidhiwa fomu na kuendelea na ujazaji na uwasilishaji. Niwapongeze Mwenyekiti wa Chama, Katibu, Sekretarieti na watumishi wengine kwa maandalizi bora,” ameongeza.