Featured Kitaifa

DKT. OMAR AZINDUA MAFUNZO YA UBAINISHAJI NA UPIMAJI WA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM

Written by mzalendoeditor

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua mafunzo ya kujengea uwezo timu za ubainishaji na upimaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ya kielimu kwa ngazi ya mikoa, yakihusisha wataalamu zaidi ya 220 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Akizindua mafunzo hayo, leo 1 Julai 2025 Mkoani Morogoro Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omar amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo, Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi, pamoja na miongozo mbalimbali ya elimu jumuishi inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wote

Dkt. Omar amesema Mafunzo hayo yanawashirikisha wataalamu wa elimu maalum, afya na ustawi wa jamii, wathibiti ubora wa shule, pamoja na wakufunzi kutoka vyuo vya ualimu visivyotoa kozi za elimu maalum.

Ameeleza kuwa Lengo kuu ni kuwawezesha wataalamu hao kutambua na kupima wanafunzi wenye changamoto mbalimbali kama vile usikivu, uoni hafifu, ulemavu wa akili, usonji, matatizo ya mawasiliano na ulemavu viungo.

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika elimu maalum ikiwemo ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi, ununuzi wa vifaa saidizi kama vile mashine za breli, viti mwendo, fimbo nyeupe, vifaa vya kusikilizia na tableti za kidijitali” Amesema Dkt. Omar.

Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara hiyo, Dkt. Margret Matonya amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa elimu maalum na yanalenga kuwawezesha wataalamu wa vituo jumuishi kuwabaini mapema watoto wenye mahitaji maalum na kuwahudumia ipasavyo.

Naye Mkurugenzi wa Elimu Msingi, Bw. Abdul Maulidi, amesema kuwa kupitia mitaala mipya ya elimu, elimu maalum imepewa kipaumbele kikubwa ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.

β€œWatoto wote, bila kujali hali zao au walipo, wanapaswa kupata elimu bora na yenye tija kwa maisha yao” ameeleza Maulid.

About the author

mzalendoeditor