Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katika kuhakikisha Wizara na Taasisi zote nchini zinatumia mifumo ya kidigitali katika utoaji wa hudumu Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kutoa huduma zake kupitia mifumo hiyo ukiwemo mfumo wa kusajili utetezi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na mfumo wa kusajili wasaidizi wa sheria.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Abdulrahman Msham, wakati wa zoezi la kuhitimisha rasmi maadhimisho hayo yaliyoanza Juni 16, 2025 na kutamatika Juni 23,2025 katika viwanja vya Chinangali Park.
Aidha, amesema jumla ya wananchi 231 waliotembelea katika Banda la Wizara ya Katiba na Sheria wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma walikuwa na changamoto za migogoro ya Ardhi, mirathi na migogoro ya ndoa.
“Katika idadi ya watu tuliowahudumia, wenye Migogoro ya Ardhi walikua wengi, wakifuatiwa na mirathi na ndoa, na hata katika kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyotekelezwa Nchi nzima, takwimu ya migogoro ya Ardhi ni kubwa ikifuatiwa na mirathi na ndoa” amesema.
Sambamba na hilo ameahidi kuwa wizara ya katiba na sheria itahakikisha inaitatua migogoro hiyo ili wananchi waishi kwa usalama.
“Kama wizara ushiriki wetu hapa pamoja na kuonesha nini wizara inakifanya lakini imeendelea kutoa huduma zake kwa wananchi ambao wametembelea banda letu na tangu tuanze hadi leo jumla ya wananchi 231 wame hudumiwa katika banda hili wakipatiwa huduma ya ushauri wa kisheria,” amesema.
Hata hivyo amesema wizara hiyo imejipanga kuendelea kutoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria katika maonesho mbalimbali yakiwemo maonesho ya sabasaba na nanenane mwaka huu.