Featured Kitaifa

SERIKALI ITAENDELEA KUWEKEZA KATIKA ELIMU YA AFYA SHIRIKA YA ELIMU KIBAHA ILI KUBORESHA MAZINGIRA YA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA – PROF. NAGU

Written by mzalendoeditor

OR – TAMISEMI, Pwani

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Profesa Tumaini Nagu amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ili kuongeza tija na ufanisi wa malengo ya taasisi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, wakati alipotembelea Shirika la Elimu Kibaha tarehe 17 Juni, 2025 wakati wa ziara ya kikazi kuona utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara na ofisi za wakufunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha.

“ Ofisi ya Rais-TAMISEMI inatambua kazi nzuri na bora mnazofanya hapa Shirika la Elimu Kibaha, na tunaendelea kushirikiana nanyi katika kuwekeza katika maeneo yenu ya kipaumbele hususani katika uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha. Naomba Shirika liendelee kuwa kioo katika mageuzi ya sekta elimu kwa Taifa letu, hasa katika malengo ya kuanzisha Taasisi hii ikiwemo na kozi za Afya” amesema Profesa Nagu.

Profesa Nagu amewataka viongozi na watumishi wa Shirika kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili mwanafunzi anayemaliza katika chuo hicho ajivunie tofauti na wanafunzi wengine kutokana na ujuzi na maarifa makubwa atakayokuwa amejifunza.

Aidha, Prof. Nagu aliwataka wataalamu kuanzisha kozi zenye kujibu changamoto za sekta ya Afya. “Mko kwenye eneo la kimkakati tumieni uwepo wenu Karibu na Hospitali ya Mkoa, na Barabara kuu kama fursa ya kuanzisha programu za mafunzo muda mfupi ya watumishi wa Afya mkishirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa”.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Tusekile Solile aliomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya katika chuo hicho ili watanzania wengi wapate fursa ya kusoma elimu ya afya.

Pia, Profesa Nagu, alipokea taarifa fupi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, Bw. Anathe Nnko ya uanzishwaji wa KEC na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha, Profesa Nagu alitembelea madarasa pacha mawili yaliojengwa kwa fedha za mapato ya ndani yaliyogharimu zaidi ya milioni 100 pamoja na ujenzi wa jengo jipya la maabara ya kompyuta ambalo litagharimu zaidi ya shilingi milioni 80 likikamilika ikiwa ni fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Shirika la Elimu Kibaha.

Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha, kinatoa kozi za Stashahada ya utabibu, Stashahada ya uuguzi na ukunga na kozi ya muda mfupi ya wahudumu wa Afya ngazi ya jamii.

About the author

mzalendoeditor