Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa majadiliano kuhusu “Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Sera za Umma kwa Usalama wa Chakula” katika Mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil (Itamaraty Palace) Jijini Brasilia .
….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ili kudhiti janga la njaa na umasikini pamoja na kuharakisha maendeleo ya vijijini, ni vema mataifa kushirikiana kwa pamoja kwa kuwa masuala hayo ni janga la linalovuka mipaka ya nchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipokuwa akitoa hotuba wakati wa majadiliano kuhusu “Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Sera za Umma kwa Usalama wa Chakula” katika Mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil (Itamaraty Palace) Jijini Brasilia.
Amesema madhara ya umasikini na njaa ni makubwa sana na yameathiri zaidi bara la Afrika licha ya uwepo wa rasilimali za kutosha. Amempongeza Rais wa Brazil Mhe. Luiz Inácio Lula da Silva kwa juhudi alizozianzisha kuunganisha mataifa na kuhamasisha ushirikiano huo kkujidhatiti baina ya mataifa tajiri na yale yanayoendelea.
Makamu wa Rais amesema Brazil itakua mshirika mzuri kwa nchi za Afrika katika kilimo cha mazao na maendeleo vijijini kutokana na matumizi ya teknolojia nchini humo pamoja na hatua kubwa iliyofikia katika sekta mbalimbali.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza uwepo wa sera rafiki na zinazotabirika zitakazoiwezesha sekta binafsi wakiwemo wakulima wadogo na wawekezaji katika sekta ya kilimo kuwa na uhakika wa uzalishaji pamoja na soko la bidhaa zao. Ameongeza kwamba sera zingine za kuangazia ni zile zitakazowawezesha wanawake ambao ndio wadau wakubwa wa kilimo barani Afrika kuwa na uwezo wa umiliki wa ardhi pamoja na kuwaondolea mila kandamizi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni muhimu Viongozi hususani wa ngazi za juu kusikiliza na kufanyia kazi ushauri kutoka kwa wadau wa sekta binafsi ikiwemo wakulima katika kuendeleza kilimo kama biashara. Amesema Tanzania imekuwa ikitumia Mabaraza ya Biashara ambayo huanzia ngazi za Wilaya hadi Taifa kwa lengo la kusikiliza changamoto na mapendekezo yanayotolewa na sekta binafsi katika kuboresha sera mbalimbali.
Makamu wa Rais ametaja mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kuangaziwa katika kukabiliana na njaa na umasikini ikiwemo vita na migogoro ya kisiasa, mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa miundombinu muhimu kwaajili ya kilimo kama vile umwagiliaji, uhifadhi mazao pamoja na TEHAMA ambayo husaidia taarifa muhimu za mbegu, masoko na bidhaa za kilimo.
Ametaja changamoto zingine za kuangaziwa kama vile ukosefu wa ufadhili katika sekta ya kilimo, changamoto ya kuuza malighafi ambazo hazijaongezwa thamani, uwekezaji katika utafiti na maendeleo, kukosekana kwa taarifa muhimu katika sekta ya kilimo, changamoto za kiteknolojia katika nyanja zote za uzalishaji pamoja na changamoto ya sera za ushuru na biashara ambazo hazihamasishi kukua kwa kilimo na shughuli za kilimo.
Majadiliano kati ya Brazil na Nchi za Afrika ni ya pili katika mzunguko wa majadiliano ya namna hiyo, ambapo majadiliano ya kwanza yalifanyika mwaka 2010 nchini Brazil. Majadiliano hayo huandaliwa na Serikali ya Brazil kupitia Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kiufundi la Brazil (ABC) Pamoja na Shirika la Utafiti wa Kilimo la Brazil (EMBRAPA).
Majadiliano hayo huwaleta pamoja Viongozi wakuu wa Serikali, Mawaziri wa Kilimo kutoka Afrika, Mashirika ya Kimataifa kama FAO, IFAD, WFP, Benki ya Dunia pamoja na wataalamu na washirika wa kiufundi. Kadhalika majadiliano hayo yametoa fursa ya kipekee ya kuangazia maeneo ya ushirikiano chini ya Mpango wa Kimataifa dhidi ya Njaa na Umaskini (Global Alliance against Poverty and Hunger) uliozinduliwa kwenye Kikao cha G20 Novemba 2024, jijini Rio de Janeiro, pamoja na kujadili mafanikio ya moja kwa moja katika sekta za kilimo, usalama wa chakula na lishe, ushirikiano wa kiufundi na biashara ya kimataifa.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula Dkt. Hussein Omar Pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Brazil Mhe. Balozi Dkt. John Simbachawene.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa majadiliano kuhusu “Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Sera za Umma kwa Usalama wa Chakula” katika Mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil (Itamaraty Palace) Jijini Brasilia .
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Temesgen Tiruneh Dinku mara baada ya majadiliano kuhusu “Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Sera za Umma kwa Usalama wa Chakula” katika Mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil (Itamaraty Palace) Jijini Brasilia .