Featured Kitaifa

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAJA NA MPANGO WA KUENDELEZA SEKTA YA UFUGAJI NYUKI

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,akiwasilisha leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma  hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA  kuhakikisha kuwa jamii inaendelea kushiriki kwenye uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za misitu na nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii  imekamilisha maandalizi ya Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyo Bora.
Mpango huo umetangazwa   leo bungeni  Mei 19,2025  na Waziri wa Wizara hiyo Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya  mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri huyo amesema Mpango huo unalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 33,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 ifikapo Juni, 2035 na kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki katika masoko ya kikanda na kimataifa.
 Aidha, Mpango unatarajiwa kuongeza ajira mpya 43,055 kupitia shughuli zilizopo katika mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki. Mpango 55 utatekelezwa katika kipindi cha miaka 10 kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara. 
Sambamba na hilo, Wizara imeandaa na kusaini Hati ya Makubaliano ya usimamizi wa mradi wa ufugaji nyuki kati ya Wizara, WAGA WMA na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. 
“Kwa lengo la kuongeza wigo wa biashara ya asali, kwa niaba ya Serikali Wizara imesaini Itifaki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China inayoruhusu uuzaji wa Asali ya Tanzania nchini China.
 “Utiaji saini wa Itifaki hii umefungua milango kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuuza asali inayozalishwa nchini katika soko la nchini China,”amesema Waziri Chana
Amesema Wizara imeratibu uzinduzi wa Alama ya Asali ya Tanzania (Honey Trademark) yenye usajili TZ/T/2023/3136 uliofanyika Oktoba, 2024. 
Amesema Alama hii ni utambulisho wa asali ya Tanzania katika soko la kitaifa, kikanda na kimataifa. Kutokana na jitihada hizi za Serikali, napenda kutoa wito wafanyabiashara wa Tanzania kuendelea kuchangamikia fursa hizi ili kuweza kuongeza kipato kwa Taifa letu kupitia biashara ya mazao ya nyuki.

About the author

mzalendoeditor