Featured Kitaifa

KIJANA AMUUA BABA YAKE MZAZI BAADA YA KUMKUTA AMELALA NA MKEWE KITANDA KIMOJA

Written by mzalendoeditor
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando
***
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 32 mkazi wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga anashikiliwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kumuua baba yake mzazi Shija Robert (55), kwa kumpiga na kipande cha kuni sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kumkuta amelala kitanda kimoja na mke wake.
Tukio hilo limetokea jana usiku April 26, 2022 katika mtaa wa Mwasele Mihogoni kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga ambapo chanzo cha tukio hilo kimetajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi baada ya marehemu kukutwa akiwa amelala kitanda kimoja na mke wa mtuhumiwa.
Radio Faraja imezungumza na Mwenyekiti wa mtaa wa Mwasele Mihogoni bwana Richard Baluhi ameeleza namna alivyopokea taarifa za tukio hilo ambapo amesema mtuhumiwa huyo alienda na mke wake kumtembelea baba yake na kwamba tukio hilo lilitokea baada ya watu hao kutumia kilevi cha pombe.
“Mimi nilipigiwa simu nikaenda kwenye tukio nikaambia huyu marehemu ameuawa na kijana wake mkubwa wa kwanza kumzaa, alimtembelea baba yake yeye anaishi Ndala alikuwa na siku nne hapo kwa baba yake.  Jana walitoka kwenda kutembea walipofika wakanywa pombe wakarudi nyumbani wamelewa, ilipofika saa nne na nusu usiku kila mmoja akaenda kulala, baada ya muda mfupi huyu mtuhumiwa alitoka nje kwenda chooni kujisaidia haja ndogo”,amesema.
“Aliporudi huyo baba mtu alishanigia kwa mke wake na huyo mtuhumiwa na kwa sababu hiyo nyumba haina taa basi huyo kijana alikuwa na tochi alipomulika akamuona baba yake amelala kitanda kimoja na mke wake basi wakaanza kupigana humo ndani na baadae wakatoana nje, huyo kijana alichukua kipande cha kuni ndipo akaanza mashambulizi akampiga mpaka kufa”, ameeleza mwenyekiti Baluhi
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Polisi George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema tayari jeshi la polisi linamshikilia mtuhumiwa huyo huku likiendela kufanya uchunguzi zaidi.
Chanzo – Radio Faraja

About the author

mzalendoeditor