Featured Kitaifa

MUUNGANO UMELETA UPENDO NA UMOJA KWA WATUMISHI WA UMMA-  RC MKIRIKITI

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiongea na watumishi (hawapo pichani) wa ofisi yake leo mjini Sumbawanga mara baada ya zoezi la usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na taasisi zilizopo katika jengo la makao Makuu wakionesha vifaa vya usafi leo mara baada ya kumaliza kufanya usafi wa mazingira ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti (wa kwanza kushoto aliyevaa kofia) akiongea na watumishi wa Ofisi yake leo mjini Sumbawanga ikiwa ni maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo wameadhimisha wka kufanya usafi wa mazingira.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa)

…………………………………………………..

Na. OMM Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti leo amewaongoza watumishi wa Ofisi yake kufanya Usafi wa mazingira ya Ofisi hiyo ikiwa ni shamra shamra za sherehe ya Miaka ya 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo amesema umesaidia kuleta upendo na umoja miongoni mwa watumishi.

Mkirikiti ameshiriki zoezi hilo la usafi (26.04.2022) katika maeneo ya Ofisi yake zilizopo mjini Sumbawanga huku akisisitiza kuwa watanzania wameendelea kuwa wamoja na wenye kuheshimiana hatua inayokuza utaifa.

“Leo ni siku muhimu kuona kama watumishi tukiwa na umoja na upendo kati yetu wa Bara na wenzetu wa Zanzibar kufuatia uwepo wa Muungano wa nchi zetu mbili. Tuuenzi Muungano wetu huu ili udumu kwa vizazi vingi zaidi vijavyo” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Donald Nssoko aliwapongeza watumishi wa umma waliopo makao makuu pamoja na taasisi zilizopo kwenye jengo la mkoa kwa kujitokeza kuadhimisha sherehe za Miaka 58 ya Muungano kwa kufanya Usafi hatua inayoongoza ushirikiano miongoni mwa watumishi hao.

Nae Dkt. Uwezo Kinahi akizungumzia kwa niaba ya watumishi alieleza kuwa tukio hilo alisema anawapongeza watanzania kwa kudumisha Muungano na kuwa kitendo cha kufanya usafi siku ya leo ni mwendelezo wa kuonesha umoja wa watanzania mahala pa kazi.

Dkt. Kinahi amewasihi wananchi wa Rukwa kuendeleza mshikamano wa kidugu na wananchi wa Zanzibar ili kwa pamoja Tanzania ipige hatua zaidi ya kimaendeleo.

Watanzania leo wanaadhimisha sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

About the author

mzalendoeditor