Featured Kitaifa

DKT. MOLLEL:’TATHMINI IFANYIKE KWANINI MIRADI ILIYO CHINI YA MKANDARASI MUST KUWA NA CHANGAMOTO’

Written by mzalendoeditor

 Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel (kushoto) akipokea maelezo kutoka kaa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekelaghe kuhusu ukarabati wa wodi ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe.Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel (wa kwanza kushoto) pamoja na watendaji wengine wa Wizara ya Afya wakiingia kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe.

**********************

Na WAF – Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameitaka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara yake kufanya tathimini ya kina ndani ya wiki kwenye miradi yote iliyosimamiwa na Mbeya Contractor Bureau iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na kutoa ushauri utakaozingatia Sheria na Taratibu ili kupata ufumbuzi wa changamoto za mkandarasi.

Dkt. Mollel ametoa agizo hilo leo alipokuwa akifanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za UVIKO-19 katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili – Mirembe na kukuta hali isiyoridhisha ya ukarabati wa jengo la wodi na hosteli unaosimamiwa na Mkandarasi MUST.

“Nimetembelea miradi mingi ambayo inasimamiwa na wenzetu wa MUST, tumekwenda Songwe, Singida, Kilimanjaro leo tuko hapa Mirembe, miradi yao yote inasuasua” amesema Dkt. Mollel

Dkt. Mollel amesema kuwa amefanya juhudi za kukutana na viongozi wa MUST kujadili changamoto zinazowakabili ambapo walikiri kufanya makosa na kuahidi kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza lakini bado utekelezaji wao wa shughuli ya ujenzi hauridhishi huku muda wa ukamikishaji wa mradi huo wa Milembe ukiwa ukingoni.

Hata hivyo Dkt. Mollel amehoji kwanini kuna kuwa na changamoto ya Mkandarasi kufanya kazi ndani ya muda na kwanini amekuwa akipewa kazi nyingi na Wizara ya Afya ilihali uwezo wake wa kuzikamilisha ni mdogo na kuitaka Ofisi ya Katibu Mkuu kufanya uchunguzi wa kina ndani ya Wizara.

“Unaweza ukadhani tatizo ni MUST, lakini inawezekana tatizo ni pande zote mbili, kwanini kila mradi utamkuta MUST, uchunguzi wa kina ufanyike lakini pia tutawaomba TAKUKURU watusaidie kuona ukweli uliopo” amehoji Dkt. Mollel

About the author

mzalendoeditor