Featured Kitaifa

SERIKALI YAELEZA ILIVYOLINDA HAKI ZA BINADAMU NCHINI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora SMZ Mhe. Dk. Mwalimu Haroun Ali Suleiman amesema kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kulinda, kuhifadhi na kukuza Haki za Binadamu kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mhe. Suleiman amesema hayo leo Machi 26, 2025 Kisiwani Zanzibar wakati akifungua kikao kazi cha kupitia rasimu ya taarifa ya nchi ya utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Itifaki ya Haki za Wanawake Afrika

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pamoja na kuridhia mikataba hii ya Haki za Binadamu ni nchi inayolinda na kutetea kwa vitendo ambapo imechukua hatua mbalimbali kama ambavyo zimeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambapo imetaja Haki za Binadamu kuanzia Ibara ya 12 hadi ya 24, Vilevile Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeainisha kuanzia kifungu 11 hadi ya 25A” Amesema Mhe. Suleiman

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu wa Wizara ya Katiba na Sheria Beatrice Mpembo amesema kuwa, kikao hicho kitasaidia katika kuboresha utekelezaji wa Haki za Binadamu kufuatia michango na maoni mbalimbali ya wadau hao

Kikao kazi hicho kitafanyika kwa siku tatu ambapo asasi za kiraia 14 za Zanzibar zinashiriki ikiwemo Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu, Jumuiya ya Mawakili Zanzibar (ZLS) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THDRC Zanzibar).

About the author

mzalendoeditor