Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ili kuhakikisha kwamba TARURA haiendi kukwama kwenye utekelezaji wa ujenzi wa barabara vijijini zaidi ya Bilioni 300 zimekusanywa kutokana na Hatifungani ya Miundombinu ya barabara za Wilaya (Samia Infrastructure Bond).
Rais Samia ameyasema hayo jana wakati wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
“Tumefungua Samia Bond na CRDB kwaajili ya fedha za miundombinu hasa barabara, bondi ile tulikukusudia kukusanya bilioni 150 bahati nzuri tumekusanya zaidi ya bilioni 300”.
Amesema kwamba kutokana na fedha hizo barabara zitaenda kujengwa kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo Rais Samia alisema wameijengea uwezo wa kibajeti TARURA pamoja na Rasiliamali watu na hivyo kuiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi.
“Tumejenga barabara mpya za lami lakini tumefungua wilaya nyingi kwa barabara zinazopitika misimu yote, natambua bado kazi ipo ya ujenzi wa barabara”. Ameongeza Rais Samia.