OR-TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imepongeza ubunifu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) katika ujenzi wa daraja la kamba za chuma kwenye barabara ya Tipri, Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Mkoa wa Manyara ambalo limeondoa kikwazo kikubwa cha shughuli za kiuchumi na kijamii wakati wa msimu wa mvua.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Justin Nyamoga, ametoa pongezi hizo katika ziara ya kukagua mradi huo katika mto Mtunguli ambao umegharimu Sh. milioni 158.9 kutoka kwenye tozo ya mafuta.
Mhe. Nyamoga ameshauri TARURA kujenga kingo za daraja hilo ili kuimarisha usalama wa watembea kwa miguu na waendesha pikipiki wanaoweza kuteleza na kuanguka mtoni.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema daraja hilo la watembea kwa miguu lina uwezo wa kubeba tani 1.5 na litadumu kwa zaidi ya miaka 70 na kutoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu hiyo muhimu.
Daraja la Tipri, lililojengwa kwenye bonde la mto Mtunguli, litasaidia zaidi ya wananchi 3,900 waliokuwa wakikwama na kupoteza mawasiliano wakati wa mvua.