Featured Kitaifa

MTENDAJI MKUU TARURA AKAGUA MIUNDOMBINU YA BARABARA WILAYANI UBUNGO

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameagiza kufanyika tathimini ya matengenezo kipande korofi cha Km. 3 katika barabara ya Malamba Mawili-King’azi ili iweze kupitika muda wote.

Mhandisi Seff ameyasema hayo jana wakati wa ziara yake wilayani Ubungo ambapo aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Kibamba Mhe. Issa Mtemvu.

Alisema katika barabara hiyo yenye urefu wa Km. 7.5 ina eneo hilo korofi na yenye utelezi hivyo kuagiza ifanyiwe tathimini ya matengenezo ili iweze kupitika vizuri kwa muda wote hususan kipindi cha mvua.

Katika ziara hiyo pia aliweza kukagua barabara ya King’ong’o-Matosa-Goba yenye urefu wa Km. 3.7 na kueleza kwamba kwa Mwaka huu wa fedha itajengwa kipande cha Km.0.8 kwa kiwango cha zege maeneo korofi ambayo yamekuwa yakisumbua sana hasa wakati wa mvua.

Hata hivyo Mhandisi Seff ameagiza Mkandarasi M/s Sonco Engineering Company Limited JV Ikamba International Ltd kurudi eneo la kazi mara moja na kuendelea na kazi ya ujenzi wa barabara ili kupunguza kero kwa watumiaji wa barabara hiyo.

About the author

mzalendo