OR-TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais- TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Arusha kusimamia kwa haraka hatua za manunuzi kwa ajili ya ujenzi wa Daraja katika Korongo la Oltukai Kata ya Esilalei – Monduli ambalo usanifu wake ulishakamilika.
Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo bungeni leo Februari 14, 2025 jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Zaitun Sawai aliyeitaka serikali kufupisha taratibu za kiutawala ili ujenzi wa Daraja hilo uanze.
Akijibu swali hilo. Mhe. Katimba amesema “ Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha asimamie hatua zote za manunuzi ili ziweze kukamilika kwa wakati na ujenzi uweze kuanza mara moja kwenye eneo hili korofi kabisa la Oltukai.”
Mhe. Katimba amesema katika mwaka 2024/25 Serikali imekamilisha kwa ajili ya ujenzi wa boksi kalavati ambapo gharama zilizobainishwa ni Sh.milioni 170.
Aidha, amesema Serikali imetenga Sh. Milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa daraja kwenye korongo la Oltukai pamoja na matengenezo ya barabara kipande korofi chenye urefu wa kilometa 2.5, ambapo barabara hiyo itachongwa na kuwekwa changarawe.