Bw. Elisha Mahenda(kushoto mwenye shati jeupe), Mwanafunzi wa Mwaka Nne, Shahada ya Uandishi wa Mitandao ya Komputa na Usalama wa Taarifa, akimwelimisha jambo mteja aliyefika kupata huduma kwenye Banda la Chuo Kikuu cha Dodoma, wakati wa Maonesho yanayoendelea ukumbi wa AICC – Arusha.
…..
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amesema Chuo Kikuu cha Dodoma, kimejizatiti katika kutekeleza maagizo ya Serikali ya kuzalisha wataalamu wabobevu kwenye sekta ya TEHAMA, pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali kufanya Utafiti hususani katika maeneo yanayohusu udhibiti wa usalama, usalama wa taarifa mtandaoni pamoja na kusaidia kuunganisha mifumo ya Serikali kusomana taarifa.
Hayo ameyasema Jumanne tarehe 11 Februari 2025, wakati akishiriki Kikao Kazi cha Tano (5) cha Serikali Mtandao (e-GA), akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo.
“Kama unavyoona UDOM imedhamini na imeshiriki kwenye Mkutano huu mkubwa kitaifa, na tumekuja na bunifu kwenye teknolojia Mnembe, ili kudhihirishia watanzania kwamba tumejizatiti katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, kwa kutumia teknolojia” alisema
Prof. Razack amesema, UDOM imeendelea kufanya vizuri katika ufundishaji na kuwa miongoni mwa vyuo bora vinavyozalisha wataalamu wa TEHAMA, na kupitia mashindano mbalimbali yanayofanyika kitaifa na kimataifa, UDOM imeendelea kuwa kinara ikionyesha ubobevu wa wataalamu wake katika kuzalisha wataalamu wenye ubora na weledi hasa katika masuala yanayohusu usalama wa mitandao.
Mkutano wa Tano wa Serikali Mtandao, ulizinduliwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza e-GA kuendelea kushirikiana na Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu nchini katika kuhakikisha malengo ya Serikali Mtandao yanafikiwa, ikiwa ni pamoja na kuzalisha wataalamu wa ndani kusaidia jitihada za Serikali za kuwa na udhibiti wa vitisho vya usalama wa taarifa, na vitisho vya usalama mtandaoni.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Mwaka wa Nne kozi ya “Kozi ya Uhandisi wa Mifumo ya Komputa, Bw. Paul Nkingwa Thomas (kushoto) akizungumza na Bw. Peter Barasa (kulia), mmoja wa wateja waliotembelea Banda la UDOM kwenye maonesho ya Kikao cha Kazi cha Tano (5), Serikali Mtandao e-GA.
Bw. Elisha Mahenda(kushoto mwenye shati jeupe), Mwanafunzi wa Mwaka Nne, Shahada ya Uandishi wa Mitandao ya Komputa na Usalama wa Taarifa, akimwelimisha jambo mteja aliyefika kupata huduma kwenye Banda la Chuo Kikuu cha Dodoma, wakati wa Maonesho yanayoendelea ukumbi wa AICC – Arusha.
Wahadhiri wa UDOM, Bw. Salim Diwani (mwenye koti), na Bw. Hamisi Fereji(katikati mwenye shati jeupe, wakifurahia jambo na mmoja wa wageni Bw. Willian Haule, alipotembelea banda la UDOM.
Prof. Razack Lokina, akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wanaoshiriki maonesho wakati wa kikao kazi cha maafisa wa Serikali Mtandao.