Featured Kitaifa

SERIKALI YARAHISISHA HUDUMA YA KUBADILISHA FEDHA ZA KIGENI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Chumbuni, Mhe. Ussi Salum Pondeza, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhakikisha huduma za kubadilisha fedha zinapatikana karibu na Hoteli za kitalii Zanzibar.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF -Dodoma)

Na. Josephine Majura WF -Dodoma

Serikali imesema imerekebisha Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za Mwaka 2019 na kutoa kanuni mpya za mwaka 2023, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni nchini.

Hayo yamelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni, Mhe. Ussi Salum Pondeza, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhakikisha huduma za kubadilisha fedha zinapatikana karibu na Hoteli za kitalii Zanzibar.

Mhe. Chande alisema marekebisho hayo, yamechangia kuongezeka kwa idadi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni Zanzibar kutoka maduka 4 yenye matawi 11 hadi maduka 15 yenye matawi 35.

Alisema mabadiliko hayo yaliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 42 la Oktoba 2023, yametoa fursa kwa hoteli zenye hadhi ya nyota tatu au zaidi kuomba leseni za kufanya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kupitia Dirisha la Daraja C.

Mhe. Chande alifafanua kuwa katika utoaji wa leseni, Kanuni zimeweka madaraja matatu (3) ya maduka (Daraja A, B na C) na kupunguza mtaji unaohitajika katika kuanzisha maduka hayo.

About the author

mzalendoeditor