OR-TAMISEMI
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Dkt. Festo Dugange, amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Kilimanjaro kuwasilisha maombi maalumu ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Sonu kwenda Sawe ambayo imeharibika kutokana na mvua.
Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo Februari 10, 2025 alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe aliyetaka kujua ni lini serikali itakarabati barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Dugange alisema: “Namuelekeza Meneja wa TARURA mkoa wa Kilimanjaro na Meneja wa TARURA Wilaya ya Hai, kama hawajawasilisha maombi maalumu na tathmini ya mahitaji ya fedha, wafanye hivyo mara moja ili serikali ipeleke fedha kwa ajili ya kuirekebisha barabara hiyo.”
Katika swali la msingi, Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo, amehoji lini serikali itapeleka fedha za dharura wilayani Kishapu kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizoathiriwa na mvua za El Nino mwaka 2023/24.
Dkt. Dugange akijibu swali hilo, amefafanua kuwa serikali tayari imepeleka sh. milioni 190 katika mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya matengenezo ya dharura kwenye baadhi ya maeneo, ikiwemo barabara ya Mwamakanga – Mwanghiri yenye urefu wa kilomita 4.5 pamoja na ujenzi wa makalavati saba.
Aidha, ameeleza kuwa TARURA Wilaya ya Kishapu inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,024.66, ambapo kilomita 2 ni za lami, kilomita 405.64 ni za changarawe, na kilomita 617.02 ni za udongo. Katika tathmini ya mwaka 2023/24, serikali ilibaini kuwa Sh.Bilioni 2.55 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo.
Dkt. Dugange amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutekeleza matengenezo ya barabara zote zilizoathiriwa na mvua, kulingana na upatikanaji wa fedha.