Featured Kitaifa

UONGOZI WA WIZARA WAWASISITIZA MABALOZI KUFANYA KAZI KWA BIDII, WELEDI

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara Balozi Joseph Sokoine wakiongea na mabalozi wanne walioapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 10 Aprili 2022, (hawapo pichani) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Balozi Mindi Kasiga, (wa kwanza kulia) Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (Multilateral Co-operation) Balozi Macocha Tembele (wa pili kulia), Balozi James Bwana ambaye atakuhudumu katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (Multilateral Co-operation) – (wa tatu kulia) pamoja na Balozi Noel Kaganda ambaye anahudumu katika Chou cha Ulinzi (NDC) wa kwanza kushoto kwa pamoja wakiwasikiliza viongozi wa Wizara (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mabalozi wakisikiliza na kufuatilia maelekezo ya Uongozi wa Wizara (hawapo pichani)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Joseph Sokoine katika picha ya pamoja na Mabalozi mara baada ya kumaliza kikao 
……………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Dar
 
Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umewaelekeza mabalozi kufanya kazi kwa bidii na weledi pamoja na kuweka maslahi ya Taifa mbele katika utekelezaji wa majukumu yao.
 
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara Balozi Joseph Sokoine wakati walipokutana na mabalozi wanne walioapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 10, 2022. Uomngozi wa Wizara umekutana na mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
 
Mabalozi hao ambao ni miongoni mwa Mabalozi 23 walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Mei 22, 2021, wamekabidhiwa majukumu mbalimbali ya Wizara kwenye ngazi ya ukurugenzi.
 
Akiwaasa Mabalozi hao, Waziri Mulamula alisisitiza kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ni kiungo muhimu kati ya Serikali na dunia hivyo mawasiliano ya ndani na nje ya Wizara yafanyike kwa weledi na wakati kwa kuzingatia viwango vya  taifa na kimataifa. “Hii itasaidia sana kuendeleza diplomasia ya Tanzania hususan wakati huu ambapo Mheshimiwa Rais amefungua nchi kwenye nyanja zote” alisema.
 
Waziri Mulamula aliongeza kuwa matarajio ya Mheshimiwa Rais kwa kuwaapisha Mabalozi vijana ni kwamba wataimarisha utendaji kazi wa Wizara kuendana na kasi yake, hivyo ni muhimu kuchapa kazi bila urasimu. “Pale ambapo mnaweza kuweka ubunifu, fanyeni hivyo, leteni mawazo mapya milango yetu ipo wazi wakati wote ili tupige hatua”
 
Naye Katibu Mkuu wa Wizara aliongeza kuwa Mabalozi hao watapangiwa majukumu mengine ya kutoa mihadhara kwenye Chuo cha Diplomasia kwa watumishi wapya lakini pia Mabalozi hao wawe kiungo baina ya Taasisi zilizo chini ya Wizara na Taasisi nyingine Serikalini kama vile Chuo cha Diplomasia (CFR) na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) 
 
Kwa mujibu wa viongozi hao, vyeo vya mabalozi hao ni: Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (Director of Multilateral Cooperation), Balozi Macocha Tembele, Mkurugezi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Director of Government Communication) Balozi Mindi Kasiga, Mkurugenzi Kazi Maalum (Ambassador Special Duties), Balozi James Bwana pamoja na Mkufunzi Mwelekezi Mwandamizi  (Senior Directing Staff – Foreign) wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Balozi Noel Kaganda.

About the author

mzalendoeditor