WAZIRI wa Madini Mhe.Anthony Mavunde,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari 25 kwa Tume ya Madini ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa maduhuri leo Oktoba 21,2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amekabidhi jumla ya magari 25 kwa Tume ya Madini ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa maduhuri huku akitoa rai kwa watumishi watakaokidhiwa magari hayo kuhakikisha wanayatumia ipasavyo na kuweze kufikia lengo lililokusudiwa.
Waziri Mavunde ameyasema leo jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa magari hayo,amesema kuwa jumla ya Bilioni 18 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari na pikipiki.
Waziri Mavunde amesema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa dhamira ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuboresha utendaji kazi wa wizara na taasisi zake.
“Magari haya 25 yanaenda kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato katika mikoa ya kimadini na katika mwaka huu wa fedha katika kipindi cha siku 90 tumekusanya sh. bilioni 287 ikiwa tumevuka lengo la kukusanya sh.bilioni 241 katika kipindi tajwa,”amesema Mhe.Mavunde
Aidha ameeleza kuwa Bajeti ya wizara ya madini imeongezeka kutoka sh.bilioni 89 mwaka 2016 hadi kufikia sh.bilioni 231 mwaka huu. Jukumu tulilonalo ni kuhakikisha sekta hii ya madini inatoa mchango chanya katika ustawi wa uchumi wa Taifa kwa kuhakikisha tunaongeza kiwango cha makusanyo.
” Magari hayo yatafungwa vifaa maalumu vya kuyafuatilia ili yasitumike vibaya.hivyo watumishi watakaokabidhiwa magari hayo kuyatumia vizuri ili kufikia lengo lililokusudiwa”amesisitiza Mavunde
Hata hivyo amesema kuwa vitendea kazi hivyo vitaenda kuimarisha zoezi la makusanyo ya fedha na kuzima mianya ya upotevu wa mapato nchini.
Awali Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema serikali imekuwa ikiongeza bajeti kwa wizara ili kuhakikisha kunakuwa na vitendea kazi vya kutosha.