Featured Kitaifa

RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AKABIDHI TUZO KWA NSSF YA USIMAMIZI NA URATIBU WA HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA BINAFSI NCHINI

Written by mzalendoeditor
 
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeshinda tuzo ya Usimamizi na Uratibu wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi  nchini, wakati wa kilele cha Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika kwenye uwanja wa EPZ Bombambili, mkoani Geita. Tuzo hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba wakati wa ufungaji wa maonesho hayo.
 
Aidha, NSSF imeshinda tuzo ya mshindi wa kwanza katika kundi la Hifadhi ya Jamii na Huduma za Bima zilizotolewa Oktoba 12, 2024 na Mhe. Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, wakati wa maonesho hayo.
 
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Bw. Mshomba amesema utoaji wa huduma kidijitali umekuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha huduma za NSSF zinawafikia wanachama popote walipo, ikiwemo kufungua madai ya kuomba mafao mbalimbali.
 
Bw. Mshomba amewataka waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanasajili wafanyakazi wao NSSF pamoja na kuwasilisha michango kwa wakati, kwani hilo ni takwa la sheria na vilevile kuwezesha Mfuko kuendelea kukua na kutoa huduma bora.
 
Aidha, Bw. Mshomba ametoa rai kwa watu waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, baba lishe, boda boda, wavuvi, wakulima, wafugaji na wajasiriamali mbalimbali kujiunga na kuchangia NSSF kwa  sababu ndiyo njia sahihi ya kupunguza umasikini wa kipato na kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.
 
Naye, Bw. Omary Mziya, Mkurugenzi wa Uendeshaji, amesema Mfuko utaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA ambapo hivi sasa wanachama wanaweza kufungua madai yao kwa njia ya kidijitali bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
 
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele amesema kupitia maonesho hayo Mfuko ulifikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wachimbaji wadogo wa madini pamoja na wajasiriamali zaidi 1500 Wilayani Bukombe. “Maonesho ya madini yalikuwa fursa kwa NSSF kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi, tutoa elimu kuhusu huduma za kidijitali pamoja na fursa za nyumba na viwanja,” amesema Bi. Lulu.
 
Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Bi. Winniel Lusingu amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Ofisi ya Mkoa huo imeweka lengo la kukisanya shilingi bilioni 104 na kuwa mwaka wa fedha uliomalizika walikusanya shilingi bilioni 64. Ameshukuru ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa uomgozi wa Mkoa huo, Waajiri, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa NSSF.
 

About the author

mzalendoeditor