Kijiji cha Ikondo kilichopo Kata ya Ikondo kupata huduma za afya za daraja la kwanza baada ya Serikali kutoa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya matatu katika Kituo cha Afya cha Ikondo.
Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Ikondo baada ya kuzindua kituo hicho Prof. Mkenda amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kujengwa kwa vituo vya afya vya Kata nchi nzima ili kufikisha huduma za afya karibu na wananchi.
Ameongeza kuwa wakati Tanzania inapata uhuru haikuwa na hospitali za Mikoa lakini baada ya miaka 60 ya uhuru kuna hospitali za mikoa katika mikoa yote nchini na sasa Vituo vya Afya vinajengwa katika Kata mbalimbali nchini.
“Napenda watanzania muone haya mafanikio haya na tujivunie ikitokea mtu akakuuliza nini kimefanyika mwambie tumejena hospitali za mikoa, shule, vituo vya afya, barabara na mambo mengi na kama kuna changamoto zitafanyiwa kazi ” ameongeza Waziri huyo.
Aidha, ameongeza kuwa kila Halmashauri ina hospitali yenye hadhi ya wilaya na kwamba huduma ambazo zamani zilikuwa lazima zifuatwe nje ya nchi sasa zinafanyika nchini
Mganga Mfawidhi Charles Kehogo amesema kuwa kituo hicho kimeondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya hasa za mama wajawazito ambao walikuwa wakiifuata kilometa zaidi ya 36.
Mganga Mkuu huyo ameongeza kuwa kituo hicho ni bora na kinakidhi mahitaji kulingana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu katika Kata ya Ikondo pamoja na kuimarisha afya na ustawi wa jamii na kwamba kina uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 6,134
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Lupembe Mhe. Enock Swale amesema kuwa kwa miaka mingi Kata ya Ikondo haikuwahi kuwa na kituo cha afya wala shule ya Sekondari lakini katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita wananchi wa Kata hiyo wanashuhudia ujenzi wa shule na kituo cha afya.
Mhe. Swale ameseema tayari serikali imeshatoa fedha zaidi ya Milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kituo hicho ambapo taratibu za manunuzi zinaendelea.