Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha.
Ikiwa ni mwendelezo wa operesheni ya nchi nzima inayofanywa na kikosi cha Usalama Barabarani ili kuzuia ajali imeendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa abiria na watumiaji wa vyombo hivyo ambapo kikosi hicho kimebaini uwepo wa baadhi ya madereva wanaotumia mwanya wa usiku kuvunja sheria huku madereva na magari yakishikiriwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Akiongea katika Operesheni hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia leo septemba 20,2024 Wilayani Arumeru Mkoani Arusha Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhan Ng’anzi amesema kuwa kikosi hicho kipo katika mwendelezo wa operesheni ya masaa ishirini na nne ambayo imelenga kukagua vyombo vyote huku akiweka wazi kuwa wanakagua makosa hatarishi ikiwemo mwendokasi na ubovu wa magari.
DCP Ng’anzi ameongeza kuwa wapo katika wilaya hiyo kukagua magari ambapo amebainisha kuwa operesheni hiyo pia imelenga kukagua viwango vya ulevi kwa madereva ambao wanafanya safari zao nyakati za usiku na wale wamchana akisisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu huku akiwaomba abiria kutoshabikia mwendo ambao umekuwa chanzo cha ajali hapa nchini.
Aidha amesema kuwa baada ya Mkoa wa Arusha operesheni hiyo itaendelea katika Mkoa mwingine ili kuhakikisha watanzania wanakuwa salama muda wote wanapotumia vyombo hivyo huku akitoa wito kwa watumiaji wa vyombo hivyo kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
Nae Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema kuwa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kimepokea maelekezo ambapo amesema kikosi hicho Mkoa wa Arusha kitahakikisha kinadhibiti ajali za barabarani huku akiweka wazi kuwa wamejipanga kudhibiti matukio hayo nyakati za usiku na mchana ambapo ametoa wito kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
Abiria ambaye anatumia vyombo hivyo licha ya kupongeza operesheni hiyo kufanyika nyakati za usiku na mchana ameomba operesheni hiyo iwe endelevu ili kudhibiti ajali zinazotokea mara kwa mara hapa nchini.