Featured Kitaifa

MKONGO WA TAIFA KUUNGANISHA NCHI ZINAZOIZUNGUKA TANZANIA

Written by mzalendoeditor

 

Na Mwandishi Wetu Arusha

Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL , limesema inandelea kuwezesha nchi zinazoizunguka Tanzania kupata huduma ya Mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unao simamiwa na kuendeshwa na Shirika hilo.

Shirika hilo linajivunia Jiografia nzuri ya Tanzania inayowasaidia kuwa kituo bora cha kuziwezesha nchi za jirani kama Kenya, Msumbiji, Zambia, Burundi na Rwanda kupata huduma za Mawasiliano.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la Maonesho la Shirika hilo lililopo katika Viwanja vya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC),Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa,amesema Shirika hilo linapopeleka huduma za mawasiliano nchi za jirani ni kati ya maeneo ya kimkakati ambapo shirika liliishapanga kuhakikisha wanafikisha huduma ili kuwezesha nchi hizo kufanya shughuli zao kidigitali.

“moja ya eneo la kimkakati ambalo TTCL tunafanyia kazi ni kuhakikisha tunafikisha huduma ya Mawasiliano kwakutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano jambo ambalo tunalifanya kwa ukamilifu mkubwa,” amesema CPA Marwa

Pia CPA Marwa amesema TTCL inatoa huduma ya Mkongo wa Taifa kwa makampuni ya Sekta Binafsi ikiwemo Kampuni za simu hapa nchini ili huduma ya Mawasiliano iweze kuwafikia wananchi wote.

” Teknolojia ama Mawasiliano ni msingi wa Maendeleo ambao unaleta tija kwa jamii hasa katika maeneo ya afya, elimu, utalii, kilimo pamoja na maeneo mengine ambayo TTCL kwa kushirikiana na Sekta binafsi imewezesha Mawasiliano ambapo yanasaidia kurahisisha huduma kwa jamii,” ameeleza CPA Marwa

CPA Marwa ameeleza kuwa TTCL ili kumfikia mwananchi moja kwa moja imekuja na huduma ya Faiba Mlangoni ambapo kupitia Mkongo wa Taifa wananchi wanapata huduma ya moja kwa moja ya Mawasiliano kwa haraka, uhakika na wanapata huduma za Internet na ya kuongea bila tatizo yeyote.

Pia katika mpango mkakati wa TTCL ni kufikisha huduma ya Intaneti katika maeneo ya wazi ambapo kwa sasa wameshafikisha katika Uwanja wa Mkapa, Mlima Kilimanjaro, vituo vya SGR na maeneo ya vyuo.

CPA Marwa anashiriki Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kilichoanza Agosti 27,2024 ambapo kinatarajiwa kumalizika Agosti 30 Mwaka huu jijini Arusha.

Kikao hicho cha siku nne kilichoandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina kilifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.




About the author

mzalendoeditor