Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya vituo vya afya yanayoanzishwa kwa nguvu za Wananchi ili kufanikisha utoaji wa huduma za afya kwa Wananchi wote.
Mhe. Dkt. Dugange amesema hayo leo (Agosti 28,2024) katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti Maalumu Mhe. Rose Vicent Busiga, lililouliza kuwa ni lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Nhomolwa – Mbogwe.
Akijibu swali hilo Dkt. Dugange amesema “Katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mbogwe, ilipeleka shilingi Milioni 100 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na nyumba ya watumishi, na tayari ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje umakamilika na kituo kimeanza kutoa huduma tangu mwezi Oktoba, 2023”.
Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mbogwe imetenga jumla ya shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la Maabara na Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya kituo cha Nhomolwa.