Featured Kitaifa

WIZARA YA AFYA YAPOKEA VIFAA VYA TEHAMA VYENYE THAMANI YA MILIONI 200

Written by mzalendoeditor

Wizara ya Afya leo imepokea vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi 203,550,000 kutoka Shirika la USAID kwa kushirikiana na JHPIEGO kupitia mradi wake wa Momentum Challenge Global Leadership (MCGL).

Akiongea wakati wa hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Abel Makubi ametaja vifaa hivyo kuwa ni kompyuta za mezani (Desktops) zipatazo 75 ambazo kupitia Idara yake ya Mafunzo zitasambazwa kwenye vyuo vya kada za Afya vipatavyo sita(6) pamoja na Wizara Makao Makuu.

Prof. Makubi ameishukuru USAID kwa mchango wao mkubwa ambao utakwenda kuboresha mafunzo ya TEHAMA vyuoni na itasaidia kuzalisha wataalamu wa afya wenye ujuzi na umahiri kwenye matumizi hayo nchini.

Ameongeza kuwa vifaa hivyo pia vitachangia kuboresha huduma za mafunzo na amevitaka vyuo vyote vitakavyonufaika na vifaa hivyo kuhakikisha wanatunza na kutumia kwa shughuli zilizokusudiwa.

Hata hivyo Prof. Makubi alitumia nafasi hiyo kuwataka wakuu wa vyuo vya afya nchini kuzingatia weledi na maadili ya utumishi wa umma kwa maendeleo ya Taifa .

“Ni wakati muafaka kwenu ninyi Viongozi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa mnazingatia maadili yote ya kitaaluma ili mzalishe wataalamu wenye uwezo katika kusaidia utoaji wa huduma za afya zenye ubora.

Kwa upande wake Mwakilishi wa USAID Dkt. Patrick Swai amesema kuwa USAID itaendelea kuisaidia Wizara ya Afya katika kuboreaha utoaji wa huduma za afya nchini.

Dkt. Swai ameongeza kuwa Tanzania ni nchi mojawapo zilizopewa kipaumbele katika mpango wa kushughulikia vifo vinavyoweza kuzuilika vya wajawazito na watoto.

Naye Mkurugenzi wa Jhpiego nchini Bi.Alice Christensen amesema kuwa Shirika lake litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali na kuahidi kuwa mshirika hai katika kuleta mabadiliko katika sekta ya afya.

About the author

mzalendoeditor