Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amewataka Watumishi wa
Serikali wanaopata fursa ya kuiwakilisha nchi nje kuwa wazalendo na kufanya kazi
kwa bidii huku wakijua wao ni wawakilishi wa nchi kwenye maeneo waliyopangiwa.
Jenerali
Mabeyo ametoa rai hiyo hivi karibuni alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini
Afrika Kusini kwa lengo la kuwasalimia Watumishi wa Ubalozi huo.
Mkuu huyo wa Majeshi amesema
kuwa, watumishi wa kada mbalimbali wanaopangiwa kufanya kazi kwenye Balozi za
Tanzania au Mashirika ya Kikanda na Kimataifa wanatakiwa kutumia fursa hiyo kuiwakilisha nchi vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa maslahi mapana ya
Taifa.
“Nawapongeza kwa kuendelea
kuiwakilisha nchi yetu vizuri hapa Afrika Kusini lakini nawahimiza mchape kazi
kwa bidii na kuwa wazalendo kwa nchi yenu wakati wote”, alisisitiza Jenerali
Mabeyo.
Kuhusu
hali ya nchi, Jenerali Mabeyo amewaeleza Watumishi hao kwamba, hali ya nchi na
mipaka yote ni salama na kuwahimiza kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wote
akiwemo Mhe. Rais ili hali ya amani na utulivu iliyopo iendelee kuwepo.
Kwa
upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu
Gaudence Milanzi amemshukuru Jenerali Mabeyo kwa kutenga muda wake na
kuutembelea Ubalozi huo na kuielezea hatua hiyo kuwa ni heshima kubwa kwake
binafsi na Watumishi wote wa Ubalozi.
Kadhalika,
alimweleza kuwa hali ya ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini ni nzuri
ambapo nchi hizi zinaendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo
biashara, utalii, elimu, uwekezaji na ushirikiano katika kukuza lugha ya kiswahiili.
Aliongeza kusema moja ya jukumu kubwa la Ubalozi
ni kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Hivyo, Ubalozi unaendelea kukamilisha
mpango mkakati wa kutekeleza dhana hiyo ili kuiwezesha Tanzania kunufaika na
fursa mbalimbali zilizopo nchini humo zikiwemo za biashara, uwekezaji na masoko
kwa bidhaa za Tanzania.
Mhe.
Jenerali Mabeyo alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano
wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulihusisha pia Jamhuri ya Msumbiji
na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM)
ambao ulifanyika jijini Pretoria kuanzia tarehe 01 hadi 03 Aprili 2022.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini. |
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akizungumza kumkaribisha Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) Ubalozini. |
Mhe. Jenerali Mabeyo akizungumza |
Mkutano kati ya Jenerali Mabeyo na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ukiendelea |
Sehemu ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini wakimsikiliza Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) alipowatembelea Ubalozini hapo |
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini |
Mhe. Balozi Milanzi akimkabidhi Jenerali Mabeyo zawadi ya saa kama ukumbusho kwa kutembelea Ubalozini hapo |
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi |
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi na Mhe. Balozi Kayola |
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini |