Featured Kitaifa

VIKUNDI VYATAKIWA KUJISAJILI VIWEZE KUTAMBULIKA

Written by mzalendo
Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Khalfan Kimaro, akiteta jambo na Wakazi wa Wilaya ya Nachingwea Bi. Zaituni Salum (kushoto) na Bi. Husna Makong’o, baada ya kumalizika kwa semina ya utoaji elimu ya fedha wilayani humo mkoani Lindi ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na akiba.
Afisa Mchambuzi Hesabu Mwandamizi, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Bi. Mariam Omari Mtunguja, akizungumza wakati wa semina ya utoaji ya elimu ya masuala ya fedha kwa Wakazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na akiba.
Baadhi ya Wakazi wa Nachingwea walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba, uwekezaji, na nyinginezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Lindi.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya  Nachingwea, Bi. Amina Ally Said, akiwashukuru Wananchi wa Nachingwea mkoani Lindi,  waliojitokeza kupata elimu ya masuala ya fedha katika semina hiyo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na akiba.
Baadhi ya Wakazi wa Nachingwea walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba, uwekezaji, na nyinginezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Lindi.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Lindi)
Na: Josephine Majura, WF, LINDI
 
Vikundi mbalimbali vinavyotoa huduma za fedha zimetakiwa kusajili vikundi vyao ili viweze kutambulika rasmi na Serikali ili kupata uhalali wa kisheria na sifa ya  kupata mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
 
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Nachingwea, Bi. Amina Ally Said, alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, iliyopo mkoani Lindi kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
 
“Kuna umuhimu wa kusajili vikundi vyetu ili kuweza kusaidika kisheria pindi changamoto zinapotokea katika vikundi kama mwanakikundi atashindwa kurudisha fedha alizochukua au viongozi kugawana fedha za kikundi, lakini kama kikundi kimesajiliwa Serikali itaweza kuwasaidia Wanakikundi hao kupata haki zao”, alisema Bi. Said.
 
Aliongeza kuwa ni jukumu letu kuwahamasisha vikundi kujisajili ili wawe na sifa za kupata mikopo au fursa zozote zinapotokea serikalini kwakuwa vikundi rasmi hupewa kipaumbele.
 
Aidha, alifafanua  kuwa takwimu za vikundi vizijulikana itaisaidia Serikali kupanga mipango na mikakati yake ya kuvifikia vikundi hivyo na kuviwezesha katika mambo mbalimbali ikiwemo mitaji na ushauri wa kitalaam kwa ajili ya kuviendeleza.
 
Bi. Amina alisema kuwa hadi sasa zaidi ya vikundi 900 vimesajiliwa katika Wilaya ya Nachingwea na wanaendelea kuhamasisha vikundi ambavyo vipo lakini havijajisajili kufanya hivyo na vikundi vipya vinavyoendelea kuanzishwa kujisajili pia kabla yakuanza utekelezaji wa majukumu yao.
 
Kwa upande wa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha mkazi wa Nachingwea, Bi. Elipina Mapua, alisema kuwa kabla ya elimu hiyo walikuwa wanafanya mambo kienyeji kama kutunza fedha kwenye visanduku na kutosajili vikundi ila baada ya kupata hiyo elimu ya fedha itawasaidia kubadilisha mfumo wao wa maisha.
 
Naye Afisa Mchambuzi Hesabu Mwandamizi, kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Bi. Mariam Omari Mtunguja, aliwashukuru wananchi wa Wilaya ya Nachingwea kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo muhimu ya masuala ya fedha.
 
“Tumekutana na Wananchi wa makundi mbalimbali ikiwemo Wajasiriamali, Wafanyabiashara na vikundi mbalimbali tumetoa elimu ya fedha katika kujiwekea akiba, masuala ya mikopo, uwekezaji, kupanga bajeti, kujipanga kwenye maisha ya kustaafu.
 
Katika zoezi la kutoa elimu kwa Wananchi, Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Fedha imeambatana  na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), wakiwa mkoani Lindi watatoa elimu hiyo katika Wilaya ya Liwale, Nachingwea, Mtama, Ruangwa, Kilwa na Manispaa ya Lindi.

About the author

mzalendo