Featured Kitaifa

TANZANIA NA UINGEREZA KUPAMBANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA WATOTO

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akijadiliana jambo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mhe. Vicky Ford walipokutana jijini Dar Es Salaam na kujadiliana kuhusu tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwa na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. Vicky Ford wakifurahia jambo mara baada ya Waziri huyo kumaliza moja ya matukio katika ziara yake nchini Tanzania.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwa na Waziri anayeshughulikia Masuala ya Afrika nchini Uingereza Mhe. Vicky Ford wakisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam mbalimbali katika Kituo cha British Council jijini Dar Es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akizungumza katika ziara ya Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mhe. Vicky Ford.

Baadhi ya wadau kutoka Taasisi mbalimbali wakiwa katika ziara ya Waziri anayeshughulikia Masuala ya Afrika nchini Uingereza Mhe. Vicky Ford iliyolenga kupata suluhu ya tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM

……………………………………..

Na WMJJWM- Dar Es Salaam

Tanzania na Uingereza zimekubaliana kuweka mikakati ya pamoja kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto hasa maeneo ya
mipakani.

Hayo yamebainika tarehe 04/04/2022 jijini Dar Es Salaam wakati wa ziara ya Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mhe. Vicky Ford iliyolenga kujadiliana na kutafuta suluhu ya tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo
kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema, Uingereza imeahidi kutoa jengo Maalum kwa ajili ya kutoa huduma za pamoja kwa ajili ya kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kupata huduma za Afya, ushauri wa kisaikolojia, Msaada wa kisheria na huduma za Polisi katika eneo moja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi uwajibikaji wa pamoja unahitajika kwa wataalam mbalimbali wanaohusika na kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili ili kusaidia kutoa huduma stahiki kwa uharaka na urahisi kwa kuokoa Jamii.

“Huduma hizi zitapatikana hapa hapa katika eneo moja na hasa kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza tumekusudia kubadili mazingira na kuleta huduma za pamoja kwa wahanga wa vitendo vya ukatili katika jengo la British Council na hii itakuwa ni kwa kuanzia na maeneo haya yatasambaa kila Mkoa” alisema Dkt. Chaula

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Mhe. Vicky Ford amesema tatizo la usafirishaji haramu wa watu inaongezeka kwa kasi hasa katika mipaka hivyo kutishia ustawi wa jamii hasa watoto.

Mhe. Vicky ameeleza kuwa Uingereza ipo tayari kushirikiana na Tanzania hasa katika kuweka Mipango mikakati ya kuhakikisha tatizo la usafirishaji haramu wa watu hasa Watoto linapungua kama sio kutokomezwa kabisa.

“Usafirishaji haramu wa watu ni shida ni tatizo kubwa hasa kwa Nchi za Afrika ambazo zimekuwa njia ya kusafirisha watu kwenda nchi za Ulaya. Tudhibiti hili tuiokoe jamii yetu” alisema Mhe. Vicky

Naye Meneja Simu ya Huduma kwa mtoto 116 Thelma Dhaje amesema uwepo wa Vituo vya pamoja vya kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia itasaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu kwa waathirika wa vitendo hivyo na kuwahakikishia upatikanaji wa Haki kwa wanaofanyiwa vitendo vya ukatili.

Aidha Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Asia Mkene amesema uwepo wa Kituo cha pamoja ya kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukatili itakuwa suluhisho kwa kuhakikisha huduma zote zinapatikana kwa wakati katika eneo moja na kuharakisha utoaji huduma.

About the author

mzalendoeditor