Featured Kitaifa

WASICHANA BALEHE WAHAMASISHWA KUTUMIA DAWA KINGA ‘PrEP’ KUJIKINGA NA VIRUSI VYA UKIMWI

Written by mzalendoeditor
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akiwa katika banda la THPS linalotoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu – Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akiwa katika banda la THPS linalotoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akiwa katika banda la THPS linalotoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu
Na Kadama Malunde- Malunde 1 blog
PrEP ni dawa ya kutumia ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa watu ambao bado hawajaambukizwa na wapo katika hatari zaidi ya kuambukizwa.
Mkoani Shinyanga, Dawa Kinga ‘PrEP’ imetajwa kuwa na manufaa makubwa katika kupunguza maambukizi ya VVU kwa wasichana wa rika balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Hayo yamebainika wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Afya Mkoani Shinyanga yaliyopewa jina la Afya Code Clinic yaliyofanyika katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga kuanzia Julai 24-27,2024 yakishirikisha wadau mbalimbali likiwemo Tanzania Health Promotion Support (THPS).
 
Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (U.S. CDC), THPS inatekeleza afua mbalimbali za afya ikiwemo Mpango wa DREAMS (Huduma Rafiki kwa vijana).
Mpango wa DREAMS una lengo la kupunguza maambukizi ya VVU kwa wasichana wa rika balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, wanaoishi katika mazingira hatarishi na wanafanya ngono katika umri mdogo ili waweze kumudu gharama za maisha na kuwaepusha mabinti wa rika balehe na akina mama vijana na tabia hatarishi.
Mmoja wa wanufaika wa Huduma Rafiki kwa Vijana (DREAMS), Prisca Daudi anasema ‘PrEP’ ni salama na tangu aanze kutumia imemfanya ajiamini na kuwa na  uwezo wa kupima VVU muda wowote tofauti na hapo awali alikuwa anaogopa sana.
Mnufaika wa Huduma Rafiki kwa Vijana (DREAMS), Prisca Daudi.
 
“Dawa kinga ‘PrEP’ ni salama , inakuweka huru na kujiamini muda wote na  haina shida. Tunaendelea kuwaelimisha vijana wengine kwamba dawa hizi ni salama, hizi siyo dawa za kufubaza VVU, zinakusaidia kujikinga na maambukizi ya VVU hata kama mwenza unayeshiriki naye tendo la ndoa ana maambukizi ya VVU”,ameeleza Prisca.
 
Naye Skewa James ambaye pia ni mnufaika wa dawa kinga anaishukuru Serikali na THPS kwa kutoa huduma ya dawa kinga hali ambayo imemsaidia kutimiza malengo yake na mpaka sasa yuko salama na anaendelea kutumia dawa kinga.
Mnufaika wa dawa kinga Skewa James.
 
“Ninawashukuru THPS kwa kunijengea uwezo wa kuweza kujitambua na kufikia ndoto zangu. Ninawashauri mabinti kutumia dawa kinga kwani unakuwa salama na inakusaidia kujiamini, dawa hizi ni nzuri zinasaidia, zinakufanya utimize malengo yako”,amesema.
Akizungumza wakati wa maadhishimo hayo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewakumbusha wananchi kuwa ugonjwa wa UKIMWI bado upo na magonjwa mengine yanayoambukizwa kwa njia ya ngono ikiwemo Homa ya Ini yapo hivyo vijana wawe makini wachukue hatua za kujikinga lakini pindi wanapobainika kuwa na maambukizi ya VVU wazingatie matumizi  sahihi ya dawa za kufubaza makali ya VVU.
Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha amesema Serikali mkoani Shinyanga inashirikiana na mashirika mbalimbali ikiwemo THPS kuhakikisha huduma zote za kinga za magonjwa zinawafikia wananchi bila kupata usumbufu wowote.
“Tunashirikiana na THPS kwenye vituo vya afya ili kuhakikisha dawa kinga za VVU zinafika kwa wakati. Wito wangu kwa wananchi wa Shinyanga ni kwamba waendelee kuzitumia huduma za afya tunazozitoa ambazo zimekubalika kimataifa. Wizara ya Afya inazitambua na tunatoa huduma zote kwa kufuata miongozo ya Wizara ya Afya”,ameongeza Dkt. Mlacha.
Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter William Mlacha.
 
Dkt. Mlacha amebainisha kuwa Dawa kinga ‘PrEP’ kwa mara ya kwanza zilionekana kuwa na changamoto kubwa kwa sababu watu wengi walikuwa wanazichanganya wakijua ni dawa za kufubaza makali yaVVU, lakini baada ya kupewa elimu na kuwahamasisha wananchi watu wengi sasa hivi wanaufahamu ukweli na watu wengi hawasiti kufika kwenye vituo vya afya kupata huduma hizo.
Katika hatua nyingine Dkt. Mlacha amesema serikali imeendelea kushirikiana na THPS kutoa huduma nyingi za kupambana na VVU, magonjwa ya ngono na homa ya ini kwa kufanya upimaji na matibabu kwenye vituo vyote vya kutolea huduma ili kuwa wafikia wananchi wengi.
 
“Kuanzia Oktoba 2023 hadi Juni 2024, Serikali kwa kushirikiana na THPS mkoani Shinyanga tumefanikiwa kufikia watu 272,800 kwa huduma za upimaji wa VVU, Vijana 250 wamefikiwa kwa huduma Rafiki kwa vijana juu ya kujikinga na VVU, wanaume 48,000 wamefikiwa kwa huduma ya tohara kinga”,amefafanua Dkt. Mlacha.
Mratibu wa Programu ya Huduma Rafiki kwa vijana (DREAMS) THPS Mkoa wa Shinyanga, Julius Sipemba amesema Programu ya Huduma Rafiki kwa vijana inatekelezwa kupitia mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na THPS kwa ufadhili wa PEPFAR kupitia CDC.
Sipemba amesema dawa Kinga imesaidia mabinti kuendelea kufanya kazi zao na maisha mengine.
Mratibu wa Programu ya Huduma Rafiki kwa vijana (DREAMS) THPS Mkoa wa Shinyanga, Julius Sipemba
 
Ameeleza kuwa tangu THPS ianze kutekeleza afua ya huduma Rafiki kwa vijana , mabinti wengi wameweza kujisimamia, wapo mabinti walioanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, wapo waliokuwa hawana uwezo wa kutunza fedha lakini baada ya kuwapa elimu wengi wameacha ngono nzembe, wameepuka mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya VVU.
Amesema, THPS imesaidia sana wananchi wa Shinyanga kwa mabinti wa rika balehe na wanawake vijana na wanaume vijana kujikinga dhidi ya VVU.
 
“Programu Rafiki kwa vijana (DREAMS) , tunahusika na mabinti wa rika balehe na wanawake vijana pamoja na vijana wa rika balehe na wanaume vijana. Mradi wa DREAMS unatekelezwa na wadau tofauti tofauti ambapo THPS inatekeleza kwenye vituo vya afya katika mkoa wa Shinyanga”,amesema Sipemba.
 
 
“Tunajihusisha na kuwafuatilia na kuwasaidia mabinti wa rika balehe na wanawake vijana ambao wapo ngazi ya vituo vya afya. THPS tulitoa mafunzo ya elimu rafiki kwa vijana kwa watoa huduma 100 ili waweze kuwapa huduma mabinti wa rika balehe wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ambao hawapo shuleni”,ameongeza.
Waelimishaji rika wakiwa katika banda la THPS
 
Amefafanua kuwa wanapokuwa kwenye vituo vya afya mabalozi hao wanasaidia kwenda kwenye vitengo ambavyo mtoa huduma anaweza kuwapata wateja wanaofika kwenye kituo na kukutana nao kisha kuwaunganisha kwenye huduma rafiki kwa vijana.
“Hapa kwenye maadhimisho ya wiki ya afya tumeweza kupata mabinti wa rika balehe na wanawake vijana takribani 114 kati yao hao walipatikana mabinti 111 wenye vigezo vya kuunganishwa kwenye huduma. Mabinti na wanawake hawa tunaratajia wana changamoto nyingi”,ameeleza Sipemba.
 
“Hivyo THPS tunawekeza nguvu nyingi ili tuweze kuwasaidia na huduma tunazozitoa kama vile upimaji VVU na wanaobainika kuwa na maambukizi tunawaunganisha kwenye huduma za tiba na matunzo na 41 wasio na maambukizi na wapo katika mazingira hatarishi tumewaunganisha huduma za dawa kinga na 27 tumewapatia huduma ya uzazi wa mpango”,amesema Sipemba.
Aidha katika maadhimisho hayo ya wiki ya afya wamefanikiwa kuibua mabinti 21 ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia majumbani kati yao 8 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na vijana wanne wameweza kuunganishwa na huduma ya tohara kinga na kufanyiwa tohara kinga.
“THPS tukishawaibua hawa mabinti wa rika balehe dawa kinga zinatolewa na mtoa huduma, muelimishaji rika ambaye tumemfundisha yeye anatoa elimu ya kawaida na faida za dawa kinga, tuna takribani watu 500 katika mkoa wa Shinyanga ambao walishagunduliwa kwamba wana sifa za kutumia dawa kinga na wapo wenye uwezo wa kujielezea namna walivyonufaika na wapo wanaoishi na watu wenye VVU, wanaendelea na ndoa zao”,amesema Sipemba.
Mratibu wa Programu ya Huduma Rafiki kwa vijana (DREAMS) THPS Mkoa wa Shinyanga, Julius Sipemba akielezea kuhsu Programu ya Huduma Rafiki kwa vijana inayotekelezwa kupitia mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na THPS kwa ufadhili wa PEPFAR kupitia CDC.
Mnufaika wa Huduma Rafiki kwa Vijana (DREAMS), Prisca Daudi akihamasisha wasichana balehe kutumia dawa kinga kujikinga na maambukizi ya VVU
Mnufaika wa Huduma Rafiki kwa Vijana (DREAMS), Prisca Daudi akihamasisha wasichana balehe kutumia dawa kinga kujikinga na maambukizi ya VVU
Mnufaika wa dawa kinga Skewa James akihamasisha wasichana balehe kutumia dawa kinga kujikinga na maambukizi ya VVU
Mnufaika wa dawa kinga Skewa James akihamasisha wasichana balehe kutumia dawa kinga kujikinga na maambukizi ya VVU
Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter William Mlacha akielezea namna Serikali mkoani Shinyanga inavyoshirikiana na mashirika mbalimbali ikiwemo THPS kuhakikisha huduma zote za kinga za magonjwa zinawafikia wananchi bila kupata usumbufu wowote.
Waelimishaji rika wakiwa katika banda la THPS linalotoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu

 

Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

About the author

mzalendoeditor