Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Shinyanga
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 16.89 kwa mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya ujenzi wa Minara ya Mawasiliano.
Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa minara 117 katika Kata 113, vijiji 240 vya Mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga.
Waziri Nape amesema hayo tarehe 19 Julai, 2024 wakati akihutubia wananchi katika Kata ya Bukomela Wilaya ya Kahama, Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga wakati akitoa majumuisho ya ziara yake ya siku tano katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Ndugu zangu wa Ngokolo, ndani ya huu Mradi wa Tanzania ya Kidigitali kuna mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa Minara 758, tunapeleka Mikoa 26 ya Tanzania Bara na ndiyo maana napita mkoa kwa mkoa, na minara hii tumelenga kuwaunganisha Watanzania milioni 8.5 na wote tunataka waguswe na huduma za mawasiliano kama vile Ngokolo na maeneo mengine yalivyounganishwa na haya ndiyo maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Nape na Kuongeza;
“Katika Mikoa niliyopita ukiwemo wa Shinyanga kwenye mradi shilingi bilioni 200 na kitu za ujenzi wa minara Tanzania nzima zitatumika kupeleka hiyo minara kwenye maeneo ya vijijini, katika mikoa mitano niliyopita billioni 16.89 zimeletwa kuhakikisha hakuna Mtanzania anaachwa nje ya huduma za mawasiliano”.
Amesema katika mikoa hiyo mitano serikali imekusudia kuwafikia Watanzania 1,868,996, wakiwemo wa Kishapu ambako minara saba inajengwa ukiwemo huo wa Ngokolo uliojengwa na Kampuni ya Honora (zamani Tigo).
Waziri Nape ameipongeza kampuni hiyo ya Honora kwa kujenga mnara wenye uwezo mkubwa wa 2G,3G, 4G na 5G uliopita malengo kwa kuvifikia vijiji vitano tofauti na malengo ya awali ya kufikia vijiji viwili huku wanufaika wakiwa ni Wakazi 20,000.
Akikagua ujenzi wa mnara uliojengwa na Kampuni ya Halotel ambao Serikali imetoa ruzuku ya Sh. Milioni 145, Waziri Nape amesema Wakazi 12,100 wa vijiji vinne vya Busangwa, Mwanima, Mwajipugira na Pambe wilayani Kishapu watapata mawasiliano.