Featured Kitaifa

BILIONI 6 KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI SIHA- KILIMANJARO

Written by mzalendo

Na, Majid Abdulkarim, Siha- Kilimanjaro

Mbunge wa Jimbo la Siha (CCM) na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollell amesema Shilingi bilioni 6 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jimbo hilo huku akiahidi neema zaidi kwa wananchi hao.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ziara yake Jimboni humo katika mkutano na wananchi wa Kata ya Kandashi baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa tanki la maji Kandashi wilya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro.

Dkt. Mollel amesema bilioni 6 zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita zinaenda kumaliza changamoto ya maji katika Jimbo hilo huku akiahidi usimamizi mzuri ili dhamira ya Rais Samia ya kumtua Mama ndoo kichwani iweze kutimia na wananchi kupata Huduma ya maji safi na salama.

“Rais Samia Suluhu Hassan anazungumza kwa vitendo hivyo niwaambie wapendwa wangu maji yatasambazwa katika kata zote za hapa Siha na mimi Mwakilishi wenu nitalisimamia hilo kwa nguvu zangu zote kikubwa tushirikiane wakati wote,”amesisitiza Dkt. Mollel.

Pia amesema ataomba nyongeza ya fedha kwa Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ili ifike Sh bilioni 14 na maeneo yote yaweze kupata maji safi na salama kwa wananchi wa Siha.

Aidha Mbunge huyo amesema Wilaya ya Siha ni ya mfano kwa kuwa na miradi mingi ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa wakati na ubora wenye kuendanda na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.

Hata hivyo katika ziara hiyo Dkt. Mollel amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo, Ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Kilimanjaro, mradi wa ukamilishaji wa vyumba vya madarasa vitano katika shule ya Sekondari Lekrimuni, Shule Mpya ya Sekondari ya Ormelili na kufungua vyumba vya madarasa tisa na matundu ya vyoo katika shule ya Sekondari Nuru katika kata ya Makiwaru.

               

About the author

mzalendo