Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, akifafanua jambo kuhusu riba ya mikopo kwa Mkazi wa Manispaa ya Tabora, Bw. Shaban Jafar, baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha kwa Wananchi wa Manispaa ya Tabora iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, akieleza umuhimu wa kuweka akiba kwa Wananchi wa Manispaa ya Tabora, waliojitokeza kupata elimi ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Baadhi ya Wananchi wa Manispaa ya Tabora, wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali.
Mkazi wa Manispaa ya Tabora, Mzee Haruna Manywele, akisoma kipeperushi chenye taarifa kuhusu mikopo ambayo ni moja ya mada ambazo zinafundishwa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo iko mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa makundi mbalimbali.
Afisa Maendeleo ya Jamiii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Manispaa ya Tabora, Bi. Helena Mathias akiikaribisha Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kutoa elimu ya fedha Wananchi wa Manispaa ya Tabora, waliojitokeza kupata elimi ya fedha iliyotolewa katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Tabora)
NA: JOSEPHINE MAJULA, WF, TABORA
Afisa Maendeleo ya Jamiii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Manispaa ya Tabora, Bi. Helena Mathias, ametoa wito kwa Wananchi wa Manispaa hiyo kutumia njia rasmi kuhifadhi fedha zao katika Taasisi zilizopewa dhamana ya kutunza fedha za Wananchi.
Bi. Helena Mathias, ametoa wito huo, alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Tabora, kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Wilaya za Urambo, Sikonge, Uyui na Manispaa ya Tabora ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Fedha na kujikomboa kiuchumi.
“Tunaendelea kuwahamasisha Wananchi wetu katika Manispaa ya Tabora kama Kauli Mbiu yetu inavyosisitiza kila ukisajili kikundi lazima ufungue akaunti ili fedha za Wanakikundi ziwe salama ili kuepusha migorogo inayoweza kujitokeza endapo sanduku linalotumika kutunza fedha likapotea”, alisema Bi. Helena Mathias.
Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kuwapa elimu Wananchi wa Manispaa ya Tabora kuhusu umuhimu wa kutunza fedha kwenye Taasisi zinazotambuliwa kisheria na Serikali lakini pia zenye dhamana ya kutunza fedha za Wananchi.
Naye Mkazi wa Manispaa ya Tabora, Bw. Ezra Abisai, ameishukuru Serikali kuona umuhimu wa elimu ya fedha kufika kwa wananchi, ambapo alisema katika semina iliyotolewa, amejifunza mambo mbalimbali ikiwemo kuwa na matumizi yasiyozidi kipato ili kujiepusha na mikopo, kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji.
Kwa upande wake Mkazi wa Manispaa ya Tabora, Bi. Mwajuma Shabani, alisema kupitia elimu ya fedha aliyoipata atakua Balozi kwa Wanakikundi wenzake kuwahamasisha kuweka fedha za kikundi kwenye Taasisi rasmi inayotambulika na Serikali ili ziwe salama.
Naye Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, aliwaomba Wanannchi wa Manispaa ya Tabora waliofikiwa na elimu ya fedha katika mambo mbalimbali ikiwemo kujiwekea akiba, uwekezaji, mikopo isiyo na riba kubwa kuitumia vizuri elimu hiyo kama fursa katika kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora katika Wilaya nne za Sikonge, Urambo, Uyui na Tabora Manispaa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu.