Featured Kitaifa

WIZARA YAHIMIZA UMILIKI WA ARDHI WA PAMOJA BAINA YA WANANDOA

Written by mzalendo

Msimamizi wa Masuala ya Kijamii Bi. Tumaini Setumbi akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki upande wa kijamii na kimazingira katika mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa mradi huo tarehe 18 Juni 2024 Mkoani Dodoma.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime akifungua Mkutano wa Wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 18 Juni 2024 Mkoani Dodoma.

Na. Magreth Lyimo, MLHHSD

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umeendelea kuweka nguvu katika kuhamasisha umiliki wa pamoja baina ya wanandoa ili kuepusha migogoro ya mirathi inayoweza kutokea pindi mmoja anapofariki.

Msimamizi wa Masuala ya Kijamii Bi. Tumaini Setumbi ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, tarehe 18 Juni 2024 Mkoani Dodoma.

Amesema Wizara kupitia mradi imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umiliki wa pamoja kuanzia ngazi ya Kitaifa hadi mtu mmoja mmoja na hadi sasa mradi umefanikiwa kuongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 25 hadi kufikia asilimia 38.

‘‘Mradi unaendesha kampeni ya kama unampenda miliki nae dhumuni kuu likiwa ni kuhamasisha umiliki wa ardhi wa pamoja baina ya wanandoa lakini pia kuchochea ongezeko la umiliki wa ardhi kwa wanawake’’ ameongezea Setumbi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinatambuliwa, kinapangwa, kinapimwa na kumilikishwa ili kupunguza au kuondoa kabisa migogoro ya ardhi.

‘‘Katika Halmasahuri ya Wilaya ya Mpwapwa takribani Hatimiliki 30,059 zitatolewa katika Kata zipatazo saba ambapo kila kiongozi katika eneo lake anapaswa kushiriki zoezi kikamilifu ili kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi na kwa wananchi jukumu lao kuu ni kushiriki na kutoa taarifa sahihi zitakazohitajika na wataalamu’’ amesisitiza Fuime

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Eng. Happiness Ngalula ametoa wito kwa Madiwani, Watendaji wa Vijiji, Watendaji Kata, Maafisa tarafa katika Wilaya ya Mpwapwa pamoja na maafisa Ardhi kufanya kazi kwa ushirikiano na kutoa elimu ya ardhi kwa wananchi ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo umeendelea kuweka nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi husani juu ya masuala ya usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi, haki za makundi maalumu kama wanawake, wazee, walemavu, wafugaji na wakulima ili kuboresha usalama wa milki za ardhi.

About the author

mzalendo