Featured Kitaifa

BIL.18.5 KUTUMIKA UJENZI WA MIFEREJI YA MAJI YA MVUA MANISPAA YA TABORA

Written by mzalendo

Angela Msimbira TABORA

NAIBU WAZIRI Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Zainab Katimba amesema
serikali inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 18.47 kwa ajili ya ujenzi wa mifereji ya kupokea maji ya mvua katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoani Tabora.

Ameyasema hayo wakati akikagua athari za mvua katika mfereji wa Mwalitani (Vimajo) uliopo katika kata ya Mpela,Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoani Tabora

Amesema kuwa tayari serikali imefanya usanifu wa awali wa mifereji ya maji ya mvua na kubaini kuwa takribani mifereji yenye urefu wa kilometa 25 inahitajika kujengwa katika Halmashauri hiyo.

Ameyataja maeneo yaliyofanyiwa usanifu huo kuwa ni Mwalitani ,uledi,Kitete-Malolo na St. Philipo-Malolo iliyopo katika kata ya ngh’ambo,mwinyi na Malolo.

Mheshimiwa Katimba pia ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuhakikisha inatenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuhudumia miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mvua.

Amewataka katika kipindi hiki cha mpito kuhakikisha wanashirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA kusafisha na kuzibua mifereji iliyoathiriwa na mvua wakati serikali ikitafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Naye Mhandisi wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Tabora Subira Manyama amesema TARURA imefanikiwa ,ujenga mifereji yenye urefu wa kilometa 2.4 kwa gharama ya shilingi milioni 399.1 katika mwaka wa fedha wa 2022/~2023 kwa kutumia fedha za tozo ya mafuta na mfuko wa jimbo kwa ajili yakukabiliana na mafuriko katika kata ya Malolo na Mpela.

About the author

mzalendo